1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanasiasa mwingine aikimbia serikali ya Tshisekedi

Jean Noel Bamwenze4 Januari 2023

Mwanasiasa Jean-Claude Muyambo, Kiongozi wa chama SCODE nchini Kongo ameamua kuondoka kutoka muungano unaomuunga mkono Raïs Félix Tshisekedi.

https://p.dw.com/p/4LivR

Siku chache baada ya kuondoka kwa Moïse Katumbi kutoka muungano wa vyama vilivyo madarakani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kutangazwa kama mugombea urais mnamo Desemba 2023, kiongozi mwengine wa muungano huo amefanya vivyo hivyo. Jean-Claude Muyambo, amesema hajaona mabadiliko yoyote.


Jean-Claude Muyambo, ambaye alikuwa waziri wa masuala ya kijamii chini ya utawala wa Joseph Kabila, alitoa tangazo hilo siku ya Jumanne wakati wa mkutano wa hadhara huko Lubumbashi, mji mkuu wa mkoa wa Haut-Katanga. 

Katika tangazo hilo lililoshangiliwa na umati wa watu, Muyambo alieleza kuwa hajaona mabadiliko yoyote baina ya Union Sacrée, yaani muungano wa vyama vilivyo madarakani leo na FCC, muungano wa vyama vilivyokuwa chini ya utawala wa Joseph Kabila.

"Waache kutuzubaisha. Niliona wale mwewe wote waliotumika na Rais Kabila wakimiminika katika muungano unaomuunga Tshisekedi mkono. Yaani mimi sijaona hata mabadiliko yoyote na ndio maana nimeamua kuondoka muungano huo na hivyo, nawajulisha kuwa mimi ni mgombea wa Urais wa Jamhuri katika uchaguzi wa 2023." amesema mwanasiasa huyo.

Muyambo asema atagombea urais mwishoni mwa mwaka 2023

Wahlen in Kongo 28.11.2011
Picha: picture-alliance/dpa

Akifafanua nia yake ya kugombea urais mwezi Desemba 2023, Jean-Claude Muyambo alisema anafahamu mateso na ukosefu wa usalama unaowakabili Wakongo.

Lakini mdadisi wa masuala ya kisiasa, Anselme Kyungu, mwalimu katika Chuo Kikuu cha Kolwezi mkoani Lualaba, anasema kinachozingatiwa katika yote hayo, iwe kwa Moses Katumbi au Jean-Claude Muyambo, ni maslahi ya kibinafsi.

"Kulingana na yale tunayoyatambua katika sekta ya kisiasa tangu utawala wa Mobutu, wengi huingia upinzani kwa matumaini na maslahi yao ya kibinafsi. Na kwa hiyo ndiyo waliingia pia kutoka katika Muungano wa vyama vinavyotawala kwani ni lazima kupinga ili kulazimisha mengi wakati wa mazungumzo."

Jean-Claude Muyambo ni wakili kutoka jimbo la Lualaba huko  Katanga. Tangazo la kugombea kwake urais limejiri zaidi ya wiki moja baada ya kuanza operesheni za uandikishaji wa wapigakura kwa ajili ya chaguzi nne zinazotarajiwa hapa tarehe 20 Desemba 2023.

Nazo ni uchaguzi wa rais, ule wa wabunge wa kitaifa na wa mikoa, pamoja na uchaguzi wa manispaa.