Mwanasiasa anayeegemea China ashinda urais Maldives
1 Oktoba 2023Matokeo hayo yanatarajiwa kwa mara nyingine kuteteresha mahusiano ya visiwa hivyo vya bahari ya Hindi na mshirika wake wa jadi, taifa jirani la India.
Mohammed Muizzi aliyeongoza muungano wa upinzani wa PPM-PNC amejikingia asilimia 54.06 ya kura dhidi ya mpinzani wake ambaye ni rais wa sasa wa visiwa vya Maldives Mohamed Solih.
Muizzi anaongoza chama cha siasa ambacho kiliridhia kiwango kikubwa cha mikopo kutoka China kilipokuwa madarakani kabla ya kuchaguliwa kwa rais wa sasa mwaka 2018.
Muizzi alikuwa na dhima kubwa katika miradi ya serikali ya wakati huo chini ya rais Abdulla Yameen, iliyoshuhudia China ikitoa kitita kikubwa cha fedha kwa ujenzi wa miundombinu.
Ushindi wake unaziweka rehani juhudi za rais anayeondoka madarakani za kuimarisha mahusiano ya nchi hiyo na India, ambayo imekuwa mshirika wa siku nyingi wa Maldives.