Mwanasheria mkuu wa Trump kukabiliwa na maswali kuhusu Urusi
13 Juni 2017Swala lingine ni kutoa majibu kuhusu jukumu lake katika kutimuliwa aliyekuwa mkurungezi wa Shirika la Upelelezi la Marekani – FBI, James Comey. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mwanasheria huyo mkuu kutoa ushahidi mbele ya umma tangu kuteuliwa na rais Donald Trump na kuidhinishwa mwezi Februari mwaka huu. Kikao hicho kinafanyika wakati mivutano ya kisiasa ikiendelea katika mji mkuu wa Marekani Washington,kufuatia ushahidi wa Comey mbele ya kamati hiyo wiki iliyopita uliozungukwa na hisia kali,huku nae rais Trump akieleza kutoridhishwa na Sessions,mmoja wa watu walioshiriki pakubwa katika kampeini yake ya kuchaguliwa kuwa rais.
Utata kuhusu kutimuliwa Comey
Katika kikao hicho Alhamisi iliopita Comey alisema shirika la upelelezi la Marekani-FBI lilifahamu taarifa ambazo zingetatiza Sessions kushiriki katika uchunguzi wa madai ya Urusi kuingilia uchaguzi mkuu wa Marekani mwaka uliopita. Comey alisema atatoa maelezo zaidi katika mazingira ya faragha,na hivyo kuzua wasiwasi kuhusu kitakochoulizwa na majibu ya kikao cha leoRais Trump alimtimua kazi Comey mapema mwezi uliopita. Huku ikizingatiwa alikuwa akisimamia uchunguzi kuhusu kuwepo uwezekano wa uhusiano kati ya timu ya kampeni ya Trump na serikali ya Urusi. Kutimuliwa kwa kwake kulizua maswali kuhusu sheria kuekewa vipingamizi.Lakini Sessions ambae alipendekeza kutimuliwa Comey,huenda akatumia cheo chake kuepuka kueleza mengi mbele ya kamati hiyo ya seneti
Amri ya Trump yapuuzwa
Wakati hayo yakijiri , Mahakama nyengine ya rufaa imelipinga agizo la rais Donald Trump la kuwapiga marufuku watu kutoka mataifa sita ya kiislamu kuingia marekani.Mataifa hayo ni Iran,Libya,Somalia,Sudan,Syria na Yemen.Jopo la majaji watatu lilisema amri hiyo inakiuka sheria zilizopo za kuhusu uhamiaji .Hata hivyo mahakama hiyo mjini San Fransisco haikusema iwapo serikali inahitajika kuzipitia upya taratibu za ukaguzi kwa watu wanaoingia nchini humo. Rais Trump amekuwa akikabiliwa na upinzani mkali kwa baadhi ya maamuzi yake ambayo amekuwa akiyafanya tangu kuingia madarakani.
Mwandishi:Jane Nyingi AP/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman