1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanamke wa Ujerumani auwawa Kabul

21 Mei 2017

Mwanamke mwananchi wa Ujerumani ameuwawa mjini Kabul ambapo repoti za awali zimedokeza kwamba mauaji hayo yametokea katika mji huo mkuu wa Afghanistan wakati wa jaribio la utekaji nyara.

https://p.dw.com/p/2dKnI
Kabul Afghanistan Polizei
Picha: picture alliance/AP Photo/M.Hossaini

Wizara ya mambo ya nje wa Ujerumani imethibitisha kwamba mwanamke wa Ujerumani ameuwawa wakati wa usiku katika mji mkuu huo mkuu wa Afghanistan lakini ufafanuzi zaidi kuhusu mauaji hayo haukuweza kufamika mara moja.Mwanamke huyo hakutajwa jina wala hayakutolewa malezo ya jinsi alivyouwawa.

Najib Danish naibu msemaji wa wizara ya mambo ya ndani amesema mwanamke mmoja wa Ujerumani na mlinzi wa usalama wa Afghanistan wameuwawa wakati mwanamke mmoja wa Finland alitekwa nyara kutoka nyumba moja ya kulala wageni mjini Kabul wakati wa saa tano na nusu usiku.

Karolina Romanoff msemaji kutoka wizara ya mambo ya nje ya Finland amethibitisha kwamba raia mmoja wa Finland ametekwa nyara lakini hana ufafanuzi zaidil.Wizara ya mambo ya nje imesema katika taarifa inataka kuachiliwa huru mara moja kwa mtu huyo aliyetekwa nyara.

Scott Brestlin mfanyakazi wa kampuni yenye makao yake nchini Sweden ya Opereration Mercy ameliambia shirika la habari la Sweden TT kwamba mmojawapo wa wafanyakazi wake hajulikani alipo na wameitisha mkutano wa dharura.

Wajerumani waonywa kutokwenda Afghanistan

Afghanistan Kabul Tatort Entführung Deutsche getötet
Mvulana akiendesha baiskeli mbele ya nyumba alikouwawa mwanamke wa Ujerumani na mlinzi wa Afghanistan.Picha: Reuters/O.Sobhani

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imekuwa ikiwaonya watu kwa muda mrefu kutosafiri kwenda Afghanistan wakati huo huo serikali ya Ujerumani imekuwa ikishinikiza kuorodheshwa kwa taifa hilo kama taifa salama ili kuwezesha kurudishwa kwa wakimbizi ambao maombi yao ya kuomba hifadhi yamekataliwa.

Hakukuwa na taarifa ya mara moja kudai kuhusika aidha na shambulio hilo au utekaji nyara.Utekaji nyara umekuja kuwa tatizo kubwa nchini Afghanistan na kwa kawaida huwaathiri wananchi wa Aghanistan ambao hutekwa nyara kwa ajili ya kudaiwa kulipa fedha za kuwagombolea.Hata hiyo wageni mara nyingine wamekuwa wakitekwa nyara nchini humo ili kuzishinkiza serikali zao.

Kabul imekumbwa na makundi ya uhalifu yalioandaliwa ambayo hupanga utekaji nyara kwa nia ya kujipatia fedha za ugombozi kwa kuwalenga mara nyingi wageni na raia matajiri wa nchi hiyo na mara nyengine kuwakabidhi makundi ya waasi.

Hali inazidi kuwa mbaya

Matumizi ya nguvu yaonyesha hali kuzidi kuwa mbaya nchini Afghanistan ambayo inakabiliana na uasi wa kundi la Taliban na makundi mengine.

Taliban imedai kuhusika na mashambulizi yaliyoratibiwa katika kitongoji cha Shah Joy ilioko katika jimbo la Zabul ambalo ni pigo jengine kwa Jumuiya ya Kujihami ya NATO ikisaidiwa na vikosi vya Afghanistan.

Asubuhi ya Jumapili (21.05.2017) kundi la wapiganaji wa Taliban wakiwa na silaha nzito na nyepesi walifanya mashambulizi hayo ya kuratibiwa kwa vituo kadhaa vya ukaguzi wa polisi na kuuwa polisi 20.

Gavana wa jimbo hilo Bismillah Afghamal ameliambia shirika la habari la AFP kwamba polisi wengine takriban 15 wamejeruhiwa katika mapigano hayo. Shambulio hilo la karibuni kabisa miongoni mwa mashambulizi ya Taliban linaonyesha kuongezeka kwa nguu za uasi zaidi ya miaka 15 tokea walipotimuliwa madarakani na uvamizi wa Marekani hapo mwaka 2001.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Lilian Mtono