Mwanajeshi wa NATO auawa Afghanistan, 15 wajeruhiwa
5 Agosti 2014Chanzo kutoka duru za usalama nchini Afghanistani kimesema kuwa tukio hilo lilitokea katika chuo cha taifa cha mafunzo ya ulinzi, baada ya mgogoro kati ya mwanajeshi wa Afghanistan na maafisa wa kigeni waliompatia mafunzo.
Chanzo hicho kimesema kuna maafa na majeruhi kadhaa, bila kubainisha idadi kamili ya waliouawa. Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Afghanistana Zahir Azimi amesema katika mtandao wa twitter, kuwa gaidi alievalia sare za jeshi la taifa aliwafyatulia risasi wafanyakazi wa chuo na wenzao wa kigeni, na kwamba baadhi ya watu wamejeruhiwa.
Azimi ameongeza kuwa mshambuliaji huyo ameuawa na wanajeshi wa Afghanistana. Rais Hamid Karzai amelaani shambulizi hilo.Wizara ya ulinzi ya Ujerumani imesema Jenerali wa jeshi lake hayuko tena hatarini na anaendelea kupatiwa matibabu.
Chuo lilikotokea shambulizi hilo kinakutikana katika eneo la Qargha, umbali wa karibu kilomita 10 magharibi mwa mji mkuu Kabul, na kinaendeshwa na vikosi vya Uingereza kuwapa mafunzo maafisa wa jeshi la Afghanistan.
Katika tukio linalofanana na hilo, afisa wa jeshi la polisi la Afghanistan na mwanajeshi wa NATO walijeruhiwa katika mapigano ya silaha, nje ya ofisi ya gavana katika mji wa Gardez, alisema Zalmay Oriyakhel, mkuu wa polisi ya Pakita, amabko tukio hilo lilitokea.
Mashambulizi yanayofanywa na wanajeshi wa Afghanistan dhidi ya NATO yalifikia kilele mwaka 2012, ambapo zaidi ya wanajeshi 61 wa jumuiya hiyo waliuwa na 81 kujeruhiwa, kw amujibu wa mtandao wa Long War Journal, ambao unafuatilia migogoro.
Mwaka uliyopita idadi ilipungua hadi wanajeshi 14 na majeruhi 29 baada ya washirika wa NATO kuchukuwa hatua zilizolenga kupungua maafa. Mwaka 2013 kulikuwepo na vifo 16 katika matukio 10 tofauti yanayowahusisha wanajeshi wa Afghanistan. NATO imesema kuwa itachunguza tukio la leo.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae,ap
Mhariri: Josephat Charo