1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanaharakati Rwanda atoweka

29 Septemba 2016

Mwanaharakati wa upinzani Rwanda Illuminee Iragena anaripotiwa kutoweka kwa miezi sita na mpaka sasa hajulikani alipo. Watu wa karibu wanahofia kuwa huenda amefariki akiwa kizuizini ambako amekuwa akiteswa.

https://p.dw.com/p/2QjuO
Nembo ya Human Rights Watch

Iragena ambaye ni nesi aliondoka nyumbani kwake jion ya tarehe 26 mwezi March akielekea kazini katika hospitali ya King Faisal, lakini hakufika kazini, hali ambayo iliifanya familia yake kutoa taarifa kwa polisi ili kufanya uchunguzi wa wapi alipo lakini mpaka sasa hawajapokea taarifa yoyote kuhusu kutoweka kwake.

Katika hali inayofanana na hiyo saa kadhaa kabla ya Irageni kutokweka mwanachama mwingine kutoka chama cha upinzani cha FDU-Inkingi, Leonille Gasengayire, alikamatwa na polisi muda mchache, baada ya kumtembelea kiongozi wa chama hicho Victorie Ingabire gerezani, akishutumiwa kumpelekea kiongozi huyo nakala ya kitabu ambacho amekiandika. Polisi walimshikilia kwa siku tatu na baadaye kumuacha huru na kisha kumkamata tena Agosti 23.

Serikali ya Rwanda yatakiwa kuweka mambo wazi

Mkurugenzi wa Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch eneo la Afrika, Daniel Bekele, amesema kuwa serikali ya Rwanda inahitaji kuweka juhudi katika kufahamu ni kitu hasa kilitokea kwa Illuminee na kuwa kama yuko kizuizini Serikali inalazimika kueleza alipo na kama kuna makosa amefanya imfungulie mashitaka au umuache huru, na kama amefariki mamlaka iweke wazi pia mazingira ya kifo chake kwa umma.

Shirika hilo la kimataifa limekuwa likiweka kumbukumbu ya matukio ya watu kupotea, kukamatwa kunakochochewa na masuala ya kisiasa na kuwaweka watu kizuizini kinyume na sheria, ambako kunafanyika nchini Rwanda hasa kwa watu ambao wanashukiwa kuwa wapinzani au wale ambao wanakosoa serikali.

Iragena ambaye pia alikuwa mgombea kwa chama cha Social Democratic Party katika uchaguzi wa wabunge mwaka 2008, mara kadhaa amekuwa akimtembelea Victorie Ingabire aliyeko gerezani akitumukia kifungo cha miaka 15 kwa kosa la kupanga mipango ya kuihujumu serikali na kwa kosa la kutokukiri kuhusika katika mauaji ya kimbari.

Mumewe pia amekuwa akikamatwa mara kwa mara

Iragena ambaye pia ni mke wa Martin Ntavuka ambaye ni mwakilishi wa zamani wa FDU-Inkingi katika mji mkuu wa nchi hiyo Kigali, ambaye pia amekamatwa na polisi mara kadhaa tangu mwaka 2010 kutokana na kujihusisha kwake na masuala ya kisiasa, Julai 8 mwaka 2011 polisi iliwakamata Iragena na mumewe baada ya kwenda gerezani kumsalimia kiongozi mwingine wa chama cha upinzani

Ndugu wa karibu wa Iragena wanaamini kuwa ndugu yao yuko kizuizini akiteswa na kuna taarifa kuwa inawezekana ameshafariki, madai ambayo shirika la Human Rights Watch halijayathibitisha japo linataka kufahamu sana kuhusu wapi alipo mwanaharakati huyo

Polisi ilimkatama Leonile Gasenganyire mwezi Machi kwa tuhuma za kuhamasisha watu kufanya vurugu ikiwa ni pamoja na kupeleka kitabu kwa Igabire ambacho jina lake lilikuwa limeandikwa kwa mkono, hakupatikana na hatua na baada ya siku tatu aliachiwa huru

Ikiwa ni chini ya mwaka mmoja kabla ya nchi hiyo kufanya uchaguzi mkuu wa raisi unaotazamiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka 2017, uhuru wa kujieleza kisiasa bado umebanwa huku kukiwa na vizuizi vingi ya uhuru wa kujieleza serikai ya Rwanda inatolewa wito wa kuwa tayari kuchunguza udhalilishaji ambao umekuwa ukifanyika kwa waandishi wa habari, wapinzani na wahaharakati ikiwa ni njia ya kuandaa mazingira ya uchaguzi huru na wa haki

Mwandishi: Celina Mwakabwale

Mhariri: Mohammed Khelef