Mwanafunzi mwenye asili ya Korea kusini awauwa wanafunzi 32 Marekani.
17 Aprili 2007Kati ya wanafunzi walionusurika na muuaji huyo,12 wako katika hali nzuri sasa na tayari wanafunzi wengine 3 wameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kupokea matibabu,japokuwa 9 wapo katika hali mbaya. Wahadhiri watatu pamoja na mhadhiri mmoja wa kijerumani, ni kati ya wanafunzi 32 waliyouwawa.
Maafisa wa polisi wamedhibithisha pia kwamba muuaji huyo alikuwa mwanafunzi kwa jina Cho Seung Hui na alihusika katika visa vyote viwili vya mauaji katika chuo kikuu cha ufundi cha Virginia. Maiti yake ilipatikana miongoni mwa mili ya wahanga katika darasa moja.
Lakini suala linalokera huko Marekani kwa sasa ni jinsi maafisa wa polisi walivyodaiwa kutokipa kisa hicho uzito uliostahili, hasa baada ya tahadhari kutolewa kutoka upande mmoja wa chuo hicho, ambapo muuaji huyo alianza kufyatua riasai na kuwauwa wanafunzi watatu.
Ripoti za polisi zimedhihirisha kwamba muuaji huyo alianza kufyetua risasi saa moja asubuhi katika bweni moja ambapo mulikuwemo wanafunzi mia tisa.Kisha masaa mawili baadaye akavuka hadi upande mwengine wa chuo hicho na kuwafyatulia risai wahanga 30 wa kisa hicho.
Baadhi ya wanafunzi wameripotiwa kukasirishwa na hatua ya maafsia hao kuwatumia onyo kwa njia ya barua pepe kuliko kuwatangazia wazi wanafunzi hao kuchukua tahadhari. Hasa baada ya baadhi ya wanafunzi waliomuona kusema kuwa hakuwa na haraka yeyote,alikuwa mtulivu kana kwamba alijua alichokuwa akikifanya,na kwa mwenendo wake wa taratibu polisi walikuwa na muda wa kumzuia. Hata hivyo maafisa wa polisi wa Virginia wamesema walichukua hatua muafaka za kiuslama kukabiliana na kisa hicho.
Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair ametuma salamu zake rambirambi kwa familia na serikali ya Marekani,akikitaja kisa hicho kuwa cha kusikitisha kwa kupoteza vijana wengi wasio na hatia. Huku huzuni zikizidi kutanda katika eneo hilo la Virginia, Rais George Bush alihudhuria kongamano la kuwakumbuka wahanga waliofariki
Zaidi ya watu elfu thelathini hufariki kutokana na majeraha ya risasi kila mwaka huko Marekani, na ripoti zinadhihirisha kuwa Marekani ndio nchi ilio na idadi kubwa zaidi ya watu wanaomiliki bunduki kuliko nchi zengine. Lakini wanaharakti wanaopinga hatua za kuondoa umilikaji wa bunduki wamesambaratisha juhudi za serikali za kudhibiti silaha kwa raia wake.
Wachanguzi wa masuala ya jinai wanasema,utamaduni wa kumiliki bunduki umewafanya wenyeji wa Marekani waone kwamba kuondoa uwezo wa kumiliki bunduki ni sawa na kuwanyima haki za kimsingi.