Mwanadiplomasia wa Algeria ziarani Afrika Magharibi
23 Agosti 2023Mwanadiplomasia mkuu wa Algeria ameanza leo ziara ya nchi za Afrika Magharibi katika jaribio la kutafuta suluhisho kufuatia mapinduzi katika nchi jirani Niger. Algeria inapinga uingiliaji wowote wa kijeshi katika mzozo wa nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Algeria Ahmed Attaf amepewa jukumu na Rais Abdelmadjid Tebboune kufanya ziara ya kidiplomasia nchini Nigeria, Benin na Ghana.
Wizara ya Mambo ya Kigeni imesema waziri Attaf anatarajiwa kufanya mashauriano kuhusu mzozo wa nchini Niger na mbinu za kukabiliana nao na wenzake katika nchi hizo za Afrika Magharibi, ambazo zinaunda sehemu ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi - ECOWAS.
Umoja wa Afrika umesitisha uwanachama wa Niger hadi pale utawala wa kiraia utakaporejeshwa na kusema utatathmini athari za uingiliaji wowote wa kijeshi.