1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka wa uchaguzi waanzia kaskazini mjini Hamburg

21 Februari 2011

Chama cha SPD chajipatia ushindi mkubwa katika uchaguzi wa kwanza kati ya sabaa za mwaka huu nchini Ujerumani.CDU kimeshindwa vibaya sana huko Hamburg

https://p.dw.com/p/10L54
Wafuasi wa SPD washangiria ushindi

Kwa kujikingia asili mia 48 nukta tatu ya kura, chama cha Social Democrat,kinachokalia viti vya upinzani katika bunge la shirikisho mjini Berlin,kimejikingia wingi mkubwa wa viti kuweza kuongoza peke yao serikali katika mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Ujerumani.Hayo ni kwa mujibu wa matokeo ya muda.

Chama cha Christian Democratic cha kansela Angela Merkel,kimachoongoza serikali kuu ya muungano katika daraja ya taifa,kimejikingia asili 21.9 ya kura-kiwango cha chini kabisa kilichowahi kujipatia katika historia yake huko Hamburg.

Kwa hivyo SPD wamerejea tena katika ngome yao iliyowaponyoka miaka kumi iliyopita,baada ya kuidhibiti kwa miaka 44.

Flash-Galerie Hamburg Bürgerschaftswahl
Diwani mpya wa Hamburg Olaf Scholz na mkewePicha: dapd

Hata hivyo anaepepea bendera ya SPD huko Hamburg ,waziri wa zamani wa ajira wa serikali kuu,Olaf Scholz anasema:

"Wananchi wengi,wake kwa waume wametuamini.Tunathamini sana hali hiyo.Inamaanisha tutafanya kila la kufanya,yote tuliyoahidi kabla ya uchaguzi kuyatekeleza pia kivitendo siku za mbele.Wote waliokipigia kura chama cha SPD,wengine pengine kwa mara ya kwanza,wanategemea majibu thabiti pia kutoka kwetu.Jibu langu ni thabiti:sitakuvunjeni moyo-yote tuliyoahidi kabla ya uchaguzi tutayatekeleza."

Chama cha CDU kimepoteza karibu ya nusu ya kura ilizojikingia katika uchaguzi kama huu mwaka 2008 huko Hamburg.

Katika wakati ambapo mwenyekiti wa chama hicho,kansela Angela Merkel hajasema kitu hadi sasa,katibu mkuu Hermann Gröhe amekiri akisema" hili ni pigo kubwa" na diwani anaemaliza wadhifa wake Christoph Ahlhaus ameungama na kusema" hakuna cha kuficha."

Walinzi wa mazingira wamejikingia asili mia 11.2 huku waliberali wa FDP wanarejea tena katika bunge la Hamburg kwa kujipatia asili mia 6.6.Chama cha mrengo wa shoto-Die Linke kimepata asili mia 6.4.

CDU-Spitzenkandidat Christoph Ahlhaus
Meya anaemaliza wadhifa wake Christoph AhlhausPicha: dapd

Pigo hilo litazidi kukibana chama cha kansela CDU kwasababu kinapoteza wakati huo huo sauti tatu katika baraza la wawakilishi wa majimbo.SPD wanaweza kuzuwia miswaada kadhaa ya sheria isipite katika taasisi hiyo.

Kushindwa CDU katika mji huo mkubwa wa bandari wa kazkazini-mahala alikozaliwa kansela Angela Merkel,ni pigo la pili mfululuzo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2009.May mwaka jana,CDU walipigwa kumbo pia katika jimbo la North Rhine Westphalia.

Chaguzi nyengine za majimbo zitaitishwa pia katika jimbo la kusini magharibi la Baden-Wurtemberg-March 27 ijayo.

Mwaka wa uchaguzi utamalizikia Berlin ambako chama cha SPD kinaweza kushindwa na walinzi wa mazingira.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir :dpa/afp

Mpitiaji:Abdul-Rahman Mohammed