1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka mmoja wa halmashauri ya haki za binadamu: Metokeo ni yapi?

Maja Dreyer19 Juni 2007

Leo ni mwaka mmoja tangu halmashauri ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imekutana mara ya kwanza. Halmashauri hiyo imechukua nafasi ya kamati ya zamani ya haki za binadamu, ambayo ilitumiwa vibaya na mataifa yaliyokiuka haki za binadamu. Mwaka mmoja baada ya kuundwa kwake, halmashauri hiyo sasa imekubaliana juu ya utaratibu wa kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/CHkV
Uwanja wa mikutano wa halmashauri ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu
Uwanja wa mikutano wa halmashauri ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za binadamuPicha: picture-alliance/ dpa

Yaliyokubaliwa ni msingi wa taratibu zitakazotumika kuanza uchunguzi dhidi ya serikali za nchi ambazo zimekiuka haki za binadamu. Hadi jana usika, China ilijaribu kubadilisha masharti ikidai kuwa uchunguzi utaanzishwa tu ikiwa theluthi mbili ya wajumbe wote 47 wa halmashauri hiyo wameunga mkono. Hadi sasa inabidi nusu ya wajumbe wakubali uchunguzi ufanyike.

Baadaye usiku, mwenyekiti wa halmashauri, Luis Alfonso de Alba wa Mexiko aliarifu kuwa maafikiano yalifikiwa ambayo yanasema pendekezo la kufanya uchunguzi kwanza liungwe mkono na wajumbe wasiopungua 15 kabla ya kupiga kura katika halmashauri. Mbele ya waandishi wa habari, Bw. Alba alisema ilibidi kuridhiana. Makubaliano si mazuri sana.

Mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanatetea haki za binadamu, baada ya mwaka mmoja wa halmashauri mpya ya Umoja wa Mataifa kuanza kazi zake, hayaoni sababu kubwa ya kufuharia halmashauri hiyo. Adrien Claude Zoeller ni wa shirika la “Geneva for Human Rights”, naye anasema mambo hayakubadilika. Wale walifanya makosa katika kamati ya zamani ya haki za binadamu, wanahudhuria zaidi katika halmashauri mpya. Amesema: “Tatizo la msingi halijatatuliwa. Wamepitisha tu sheria fulani ili kuonyesha kwamba nchi ziwe na wasiwasi pindi zikikiuka haki za binadamu. Serikali haziwezi tena kutojali haki za binadamu. Hapa tu, hali imeboreka kiasi.”

Katika muda huu wa mwaka mmoja, halmashauri hiyo ya haki za binadamu imekutana mara nane. Mikutano mitatu ilishughulikia suala la mzozo kati ya Israel na Wapalestina. Kama ilivyokuwa hapo awali, kulikuwa na mgawanyiko ndani ya halmashauri. Kwa upande mmoja kuna nchi za Magharibi, na kwenye upande mwingine nchi za Kiislamu. Mwanzo haukuleta matokeo mengi, anasema Peggy Hick wa shirika la “Human Rights Watch”: “Lakini kulingana na tathmini yetu, angalau kuna msingi, ila tu ni dhaifu. Inabidi kufanya kazi nyingi ili kamati hiyo mpya iweze kutekeleza ahadi zilizotolewa.”

Bi Hicks lakini aliongeza kusema kuwa masharti yalivyo hivi sasa yanaziruhusu nchi kudhoofisha ulinzi wa haki za binadamu.

Leo hii, halmashauri ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za binadamu iliarifu pia kuwa nchi mbili, yaani Cuba na Belarus, zimetolewa kwenye orodha ya nchi ambako hali za haki za binadamu inachunguzwa kwa kina. Halmashauri hiyo itaweza pia kutuma wajumbe maalum watakaokagua hali ilivyo.

Kamati ya zamani ya haki za binadamu ilikosolewa kwa sababu nchi fulani ambazo zilijulikana kutoheshimu haki za binadamu zilikuwa wanachama. Halmashauri mpya ilitangaza kuwa itafuta mashaka haya. Licha ya masharti makali zaidi ya kuwa wanachama, lakini bado mataifa fulani yaliyotiliwa shaka katika halmashauri hiyo, kama vile Cuba, Saudi-Arabia na China.