1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka mmoja madarakani, mikakati ya Obama Mashariki ya Kati yafanikiwa?

Kabogo Grace Patricia13 Januari 2010

Alipoingia madarakani Rais Obama aliahidi kuyashughulikia matatizo katika Mashariki ya Kati ikiwemo kuwaleta katika meza moja Wapalestina na Waisraeli.

https://p.dw.com/p/LV7x
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: AP

Ikiwa ni mwaka mmoja sasa tangu Rais Barack Obama wa Marekani alipoingia madarakani Januari 20, mwaka uliopita wa 2009, kiongozi huyo aliahidi kuyashughulikia matatizo katika Mashariki ya Kati, yakiwemo matumaini ya kuwaleta pamoja Waisraeli na Wapalestina.

Katika siku yake ya kwanza ofisini, Rais Obama alianza kujihusisha na amani ya Mashariki ya Kati wakati alipowapigia simu viongozi wa eneo hilo na siku ya pili kumteua George Mitchell kuwa mjumbe maalum katika Mashariki ya Kati, ambaye wiki moja baadaye alifanya ziara huko Jerusalem na Ramallah. Tangu wakati huo, juhudi za amani hazijaendelea hata kwa kiasi kidogo. Baada ya mazungumzo ya amani kuvunjika Desemba, mwaka 2008, pande hizo mbili bado hazijarejea katika meza ya mazungumzo. Kitu kikubwa kinachokwamisha mazungumzo hayo ni serikali ya Israeli ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kutaka kurejea katika mazungumzo hayo bila kuwekewa masharti yoyote yale. Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas anataka kusimamishwa kwa ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki kabla mazungumzo hayajaanza tena.

Profesa Eytan Gilboa wa taaluma ya siasa nchini Israel alitakiwa na shirika la habari la Ujerumani-DPA- kutathmini mikakati ya Rais Obama katika Mashariki ya Kati. Profesa Gilboa alimpa Rais Obama daraja la pili katika kumi, ambapo anasema kiongozi huyo wa Marekani alikosea kuliweka suala la ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kama ajenda kuu ya mjadala huo. Kwa upande wake, mchambuzi wa Palestina, Profesa Hani Masri, anasema Rais Obama ameshindwa katika awamu ya kwanza. Hata hivyo, anaukosoa uongozi wa Palestina, akisema tangu wakati huo, Abbas ametangaza kutogombea katika uchaguzi mwingine wa urais. Msemaji wa serikali ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi, Ghassan Khatib, anasema ingawa Rais Obama hakufanikiwa kupata ufumbuzi, alifanikiwa kuleta mabadiliko chanya ya msingi katika sera za Marekani kuelekea Mashariki ya Kati. Ghassan Khatib anasema Rais Obama amefanikiwa kuonyesha kujihusisha kwake na amani ya Mashariki ya Kati kuliko alivyofanya mtangulizi wake.

Kiongozi wa kundi la Hamas katika Ukingo wa Magharibi, Ismail Radwan, ameliambia shirika la habari la DPA kuwa Rais Obama amebadilisha ahadi zake kwa Waarabu, Wapalestina na Waislamu. Radwan anasema baada ya mwaka mmoja, badala ya kuishinikiza Israel kuhusu uvamizi, Rais Obama ameelekeza shinikizo lake katika upande wa Palestina. Marekani sasa inajaribu mbinu mpya ya mipaka kwanza na makaazi baadaye. Mjumbe maalum katika Mashariki ya Kati, George Mitchell, amesema anatumai kuzisukuma pande hizo kuelekea katika maazimio ya masuala ya mipaka kabla ya kusimamishwa kwa muda ujenzi wa makaazi. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jordan, Nasser Judeh, ambaye pamoja na waziri mwenzake wa Misri wanajaribu kumshawishi Abbas kukubali mfumo mpya wa Marekani, akielezea muda wa kikomo. Waziri Judeh anasema wana michakato mingi, lakini hakuna amani ya kutosha.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPA)

Mhariri: Miraji Othman