1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwa kilele wa APEC

5 Septemba 2007

Rais wa Marekani, George Bush, amewasili Sydney, Australia, kuhudhuria mkutano wa kilele wa nchi za Asia na zile zilioko katika Bahari ya Pasifik akisema bado uamuzi wa mwisho haujafikiwa kuhusu idadi ya wanajeshi wa Kimarekani watakaobakia Iraq. Wakati huo huo, wanaharakati wenye kupinga vita walishindwa leo mahakamani kuhusu takwa lao la kufanya maandamano katikati ya mji wa Sydney kupinga siasa za Marekani katika Iraq.

https://p.dw.com/p/CH8S
Rais Bush wa Marekani na waziri mkuu wa Australia,Howard, wakiwa katika bandari ya Sydney.
Rais Bush wa Marekani na waziri mkuu wa Australia,Howard, wakiwa katika bandari ya Sydney.Picha: AP

Australia imeanzisha operesheni kubwa kabisa ya ulinzi, ikiweka ukuta wa senyenge wenye urefu wa mita 2.8 ambao umeugawa mji wa Sydney katika sehemu mbili, jambo ambalo limewakasirisha watu wa mji huo. Nchi hiyo haijawahi kushuhudia mashambulio ya kigaidi ndani ya mipaka yake. Wanaharakati wenye kupinga vita walipanga kufanya maandamano ya hadi watu 20,000 kuipinga ziara ya Rais Bush nchini humo na vita vinavoendeshwa na Marekani huko Iraq. Polisi wa Australia wana hofu kwamba makundi ya watu wachache watafanya fujo zisizowahi kuonekana nchini humo.

Lakini waziri mkuu wa Australia, John Howard, amekula kiapo kwamba atayabakisha majeshi ya nchi yake katika Iraq licha ya mbinyo anaowekewa ayarejeshe majeshi hayo nyumbani. Alisema ahadi alioitoa kwa Iraq inabakia, na sasa sio wakati wa kutolewa pendekezo lolote la kupunguza majeshi ya Australia. Aliyasema hayo katika mkutano wa waandishi wa habari uliohudhuriwa pia na Rais Bush na ambaye naye aliushukuru mchango unaotolewa na Australia katika vita vya Iraq.

Siku chache zijazo kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani katika Iraq, David Petraeus, na balozi wa nchi hiyo mjini Baghdad, Ryan Crocker, watatoa ushahidi mbele ya bunge kuhusu hali ya kijeshi na ya kisiasa katika Iraq. Rais Bush amesema mapendekezo ya watu hao wawili yatakuwa muhimu kwake yeye kutunga mkakati. Amesema masikilizano yanafanyika huko Iraq , na ni muhimu kwa usalama wa Marekani na wa Australia kwamba majeshi ya nchi hizo mbili yanabakia Iraq ili kuwasaidia watu wa nchi hiyo.

Australia ina wanajeshi 1,500 na Marekani 160,000 huko Iraq. Rais Bush alimzawadia waziri mkuu Howard kwa utiifu wake kwa kutia saini leo mkataba utakaoipa Australia ruhusa ya kujipatia teknolojia ya kijeshi ya siri kabisa kutoka Marekani. Australia kwa muda mrefu imelalamika juu ya vikwazo vilivowekwa na Marekani juu ya teknolojia ya silaha na habari kwa sababu ya wasiwasi wa Marekani kwamba teknolojia hiyo inaweza ikawafikia majasusi.

Waziri mkuu Howard alisema amezungumza na Rais Bush juu ya mpango ambao kwamba vifaa vya misaada na bidhaa kwa ajili ya kupambana na majanga vitawekwa huko Australia ambavyo vitatumiwa kwa haraka zaidi kusaidia pindi pakitokea majanga ya kimaumbile katika eneo la Kusini Mashariki ya Asia na Bahari ya Pasifik:

+Ushirikiano ulio bora katika sekta ya misaada ya kiutu unaweza ukapelekea siku za mbele vifaa na bidhaa za misaada za Marekani kuhifadhiwa katika maghala ya Australia, vitu ambavyo vinaweza kutumiwa papo hapo pindi kukitokea janga katika eneo letu. Tunafikiria hasa pindi kukitokea janga kama la Tsunami ambalo liliwahi kutokea miaka michache iliopita.+

Kuondoshwa vizingiti katika biashara na mabadiliko ya hali ya hewa duniani ni mambo yalioko juu kabisa katika ajenda ya mkutano wa kilele wa APEC huko Sydney, na Rais Bush anataka chumi za nchi 21 ziliomo katika ushirikiano huo zikubakliane kutoa ahadi za kuyapa uhai mpya mazungumzo ya Doha juu ya biashara duniani.

Mabwana Bush na Howard pia walizungumzia juu ya nguvu za Uchina katika jukwaa la kimataifa ambayo rais wake, Hu Jiantao, pia anatazamiwa kuwasili Sydney baadae leo kwa ajili ya mkutano huo. Huu Jiantao alilitemebelea shamba la kondoo karibu na mji mkuu wa Australia, Canberra. Uchina inanua sufi nyingi kutoka Autralia, na kinyume na Bush, Bwana Hu amepata mapokezi mazuri.

Mswaada wa tangazo lililotayarishwa na mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi hizo za APEC ulisema nchi hizo zitajaribu kuendeleza mismamo imara wa kuimarisha viwango vya usalama wa vyakula na bidhaa katika eneo hilo. Msimamo huo ni kuzuwia majaribio ya magaidi kutaka kuvitia sumu vyakula. Kuhusu biashara, Ushirikiano wa nchi za APEC utajishughulisha mwaka huu kuimarisha masoko ya rasil mali, kupambana na rushwa, kuendeleza utawala bora na kuweko utaratibu wa sheria na kanuni zenye kuwa na uhakika.