Mvzozo wa kidiplomasia Iran, Uingereza wazidi
1 Desemba 2011Uingereza imewaondoa mabalozi wake wote kutoka Iran na pia imeufunga ubalozi wa Iran mjini London .
Akizungumza bungeni hapo jana Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague alisema kuwa wawakilishi wote wa kibalozi wa Iran wanatakiwa waondoke Uingereza katika muda wa saa 48.
Hapo awali watumishi wote wa ubalozi wa Uingereza nchini Iran walikuwa wameshaondolewa .
Serikali ya Iran imejibu kwa kusema kwamba hatua ya Uingereza ya kuufunga ubalozi wake itakuwa na madhara.
Ujerumani na Ufaransa pia ziliwarudisha nyumbani mabalozi wao wa nchini Iran kwa ajili ya mashauriano.
Waandamanaji nchini Iran waliuvamia ubalozi wa Uingereza hapo juzi, baada ya Uingereza kuviimarisha vikwazo dhidi ya serikali ya Iran kutokana na mzozo uliosababishwa na mpango wa kinyuklia wa nchi hiyo.