Mvutano wa kibiashara watarajiwa kutawala mkutano wa G20
29 Novemba 2018Mkutano wa kilele wa nchi 20 zinazostawi kiuchumi, kundi linalojulikana kama G20, utafunguliwa kesho mjini Buenos Aires Argentina. Suala la mvutano wa kibiashara kutokana na msimamo wa Marekani kujilinda kibiashara linatarajiwa kutawala zaidi katika mkutano huo.
Kutokana na sera yake ya "Marekani kwanza," katika suala la biashara rais Donald Trump hakuvutana tu na Umoja wa Ulaya na Canada , bali pia na China. Mvutano kuhusu biashara unasababisha biashara ya dunia kuwa katika hali ya msukosuko huku mkuu wa Shirika la fedha la Kimataifa IMF Christine Lagarde ambaye atashiriki katika mkutano huo, akionya kwamba mgogoro wa kibiashara una athari kubwa kwa uchumi wa dunia, ambapo ukuaji wa uchumi wa dunia umeporomoka kwa 0.5 asilimia.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani pamoja na viongozi wengine katika kundi hilo la G20 ukimuweka kando Trump, wanatarajiwa kupigia upatu biashara huru. Kwa wakati huu kutokana na hali ilivyo, mtu anaweza kusema ingawa sio rasmi kwamba kauli mbiu ya mkutano huo wa kilele ni " sote dhini ya mmoja , sote dhidi ya Trump."
Rais Trump na Xi Jinping watarajiwa kukutana kuondoa tofauti zao
Wakati wa mkusanyiko huo wa Buenos Aires, Trump anatarajia kukutana na Rais wa China Xi jinping kujaribu kufikia makubaliano ya kuondoa tafauti zao. Lakini tayari alikwisha onya kwamba pindi itashindikana basi China iwe tayari kwa vikwazo vya Marekani, akioonya ana mpango wa kuitoza China ushuru wa jumla wa dola 250 bilioni kwa biadhaa zake zinazoingia Marekani pindi hapatokuweko makubaliano yoyote ..
Iwapo rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker atakutana kwa mazungumzo na Trump kandoni mwa mkutano huo wa kilele wa G20 bado haijafahamika wazi. mabishano na Umoja wa Ulaya ni kuhusu ushuru katika biashara ya magari kutoka nchi wanachama wa Umoja huo.
Rais Trump atarajiwa kukutana na Rais Putin
Kwa upande mwengine yamepangwa mazungumzo kati ya Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin, lakini haiko wazi ikiwa watafikia maelewano au la Akiulizwa kama mazungumzo yatavunjwa kutokana na mgogoro mpya kati ya Urusi na Ukraine, Trump aliliambia gazeti la Washington Post kwa mkato tu." Sipendi tabia ya uchokozi dhidi ya wengine."
Kandoni mwa sarakasi yote hiyo kumhusu Trump, Duru za kibalozi za Umoja wa Ulaya zinasema suala jengine litakalopewa kipa umbele katika mkutano wa Buenos Aires ni kuwashajiisha waajiri kuwa na mpango bora wa mafunzo kwa vijana utakaofungua nafasi za ajira. Hiyo ni mada muhimu kwa Afrika na suala linalopigiwa upatu na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, ambaye anasema, upande huo Ujerumani ina mchango mkubwa wa kutoa kupitia kile kinachoitwa, "Mpango kwa ajili ya Afrika, uliobuniwa wakati wa mkutano uliopita wa G20 katika jiji la kaskazini mwa Ujerumani la Hamburg, ambao Ramaphosa alishiriki.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/Bernd Riegert (DW)
Mhariri: Mohammed Khelef