1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano waendelea Ukraine

24 Januari 2014

Waandamanaji nchini Ukraine wamelivamia jengo la serikali katika mji mkuu Kiev wakati pia wakiendelea kuzizingira ofisi kadhaa za magavana magharibi mwa nchi hiyo huku mbinyo dhidi ya serikali ukiongezeka

https://p.dw.com/p/1AwTc
Ukraine Proteste in Kiew 24.01.2014
Picha: Reuters

Baada ya kukutana na rais Viktor Yanukovich katika kikao kilichodumu hadi usiku wa manane, viongozi wa upinzani waliuambia umati kuwa rais huyo aliahidi kuhakikisha kuwachiliwa huru mamia ya waandamanaji waliokamatwa baada ya makabiliano na polisi na kusitisha ukamataji zaidi.

Wamewataka waandamanaji kuheshimu agizo la kuwataka wawe watulivu kufuatia vurugu zilizozuka katika barabara za mji mkuu Kiev, katika kipindi cha wiki moja iliyopita, lakini walikemewa na waandamanaji walioonekana kukaidi wito huo. Waandamanaji wamepanua kambi yao ya maandamano na kuweka vizuizi kwenye barabara za mji mkuu baada ya mazungumzo muhimu kati ya upinzani na rais Yanukovich kushindwa kufikia makubaliano.

Wamelitwaa jumba la wizara ya kilimo katika mji mkuu huku kiongozi wa upinzani, ambaye ni bingwa wa zamani wa ndondi Vitali Klitschko akisema uwanja wa Uhuru mjini Kiev ni kisiwa cha uhuru, na kwa hivyo wataendelea kuipan ua kambi yao ya maandamano hadi watakaposikika.

Hopes for Ukraine solution

Vurugu za wiki hii, ambazo zimekuja baada ya miezi miwili ya maandamano ya kupinga hatua ya rais Yanukovich kusaini mkataba wa ushirikiano na Umoja wa Ulaya chini ya shinikizo kutoka kwa Urusi, zimeyageuza maeneo kadhaa ya mji wa Kiev kuwa uwanja wa mapambano na kusababisha vifo vya wanaharakati watano. Klitschko amesema rais anaonekana kuziba maskio nta kuhusiana na wito wa upinzani unaomtaka ajiuzulu kutoka serikalini.

Bunge linatarajiwa kukutana Jumanne wiki ijayo ili kuyajadili matakwa ya waandamanaji la kuitaka serikali ijiuzulu na pia kufutiliwa mbali sheria zinazopiga marufuku maandamano. Hofu pia imetanda nje ya mji mkuu, na gavana wa jimbo la magharibi mwa Ukraine la Lviv, Oleg Salo, amejiuzulu jana baada ya waandamanaji wanaoipinga serikali walipoivamia ofisi yake..

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden amempigia simu rais Yanukovich akimwonya kuwa kushindwa kuukwamua mzozo huo kunawezakuwa na athari mbaya. Naye Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameelezea hasira yake kuhusiana na namna sheria zinavyovurugwa na kuzusha suali la haki za uhuru, wakati Rais wa Ufaransa Francois Hollande akiwataka maafisa wa Ukraine kutafuta haraka suluhusho kupitia mazungumzo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Josephat Charo