1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wa kisiasa waendelea Zimbabwe

Nijimbere, Gregoire20 Juni 2008

Wiki moja kabla ya uchaguzi wa urais nchini Zimbabwe, chama kikuu cha upinzani cha mageuzi ya kidemokrasi MDC cha Morgan Tsvangirai, kinafikiria kujitoa kwenye uchaguzi huo kutokana na vitendo vya kukinyanyasa

https://p.dw.com/p/ENRK
Morgan Tsvangirai, kiongozi wa chama cha MDCPicha: AP

Kulingana na msemaji wa chama hicho cha MDC Nelson Chamisa, wamekuwa wakipokea shinikizo nyingi hasa kutoka kwa wafuasi wao kutoka sehemu za vijijini kwamba ingefaa wajitoe katika kile wamekitaja mchezo wa kisiasa. Hata hivyo Chamisa hajasema ni lini chama chake kitatangaza msimamo wake juu ya hilo.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu na nchi za magharibi zinamtuhumu rais Robert Mugabe na chama chake cha ZANU-PF kuchochea ghasia kuutisha upinzani kwa lengo la kuendeleza utawala wake ambao umekwisha dumu miaka 28.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleeza Rice aliwaambia wanadiplomasia kutoka nchi za Afrika mjini New York Marekani kwamba wakati umewadia jamii ya kimataifa kuchukuwa hatua dhidi ya Zimbabwe.

" Mimi sijaona kitu rais Mugabe alichokifanya kuwasaidia wananchi wake. Ninadhani umefika muda jamii ya kimataifa kutoa shinikizo“.

Umoja wa Ulaya tayari unafikiria kutangaza vikwazo dhidi ya Zimbabwe. Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ambao wanakutana mjini Brussels,Ubelgiji wanatarajia kutoa taarifa baadaye hii leo juu ya msimamo wao kuhusu Zimbabwe.

Lakini tayari mswada wa taarifa hiyo ambao umepitiwa na waandishi wa habari, unatoa mwito kwa Umoja wa Afrika na jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC kuwatuma waangalizi wa kutosha nchini Zimbabwe na zoezi la kuhesabu kura lisidumu muda mrefu kama ilivyotokea katika duru ya kwanza ya uchaguzi mwezi Machi mwaka huu.

Inaongeza kusema "Umoja wa Ulaya uko tayari kuchukua hatua zaidi dhidi ya wanaochochea machafuko".

Hadi sasa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Zimbabwe, vinahusu silaha na visa kwa mafisa wa serikali kiasi ya 100 akiwemo rais Mugabe.


Takriban wafuasi 70 wa upinzani wameshauawa na maelfu kadhaa kupigwa au kuteswa na wapiganaji wanaoaminika kuwa wafuasi wa chama tawala cha ZANU-PF na vikosi vya idara za usalama.

Hata kiongozi wa chama cha MDC Morgan Tsvangirai ambaye atashindana na rais Mugabe kwenye uchaguzi huo ifikapo tarehe 27 mwezi huu, ameshakamatwa na polisi mara 5 kwa muda wa mwezi mmoja tu uliopita na msaidizi wake Tendai Biti ambae ni katibu mkuu wa chama, bado anazuiliwa katika kituo cha polisi akikabiliwa na tuhuma za uhaini.