Mvutano ndani ya chama tawala Kenya, Jubilee waongezeka?
6 Mei 2019Naibu Rais William Ruto amewakosoa baadhi ya viongozi wa chama tawala cha Jubilee kwa madai ya kujiunga na upinzani ili kuvurugu azma yake ya kuwania kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, huku akisema kuwa hata hivyo Jubilee iko imara licha ya kuibuka makundi mawili yanayokinzana.
Salamu za heri kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, zinazidi kuzua mtafaruku katika chama cha Jubilee. Sasa pameibuka matapo mawili ndani ya chama hicho tawala: kundi la Tangatanga linalomuunga mkono Naibu Rais William Ruto na lile la Kieleweke linalompinga. Licha ya hali hiyo, Naibu Rais Ruto angali anashikilia kuwa hakuna mpasuko chamani:
"Na hiki chama sio lazima mtu fulani akiongoze, kama kutakuwa na mtu bora kuzidi Ruto, sio lazima niongoze, huyo tutamuunga mkono, lakini sote tutakuwa ndani ya Jubilee. Kile ambacho hatutakubali ni kuletewa fitina za vyama vingine."
Ukimya wa rais Kenyatta wasababisha mpasuko?
Wachambuzi wanasema kuwa mpasuko unaoonekana katika chama tawala, umesababishwa na ukimya wa Rais Kenyatta kuhusu mrithi wake na badala yake kushirikiana na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga. Waungaji wa makundi haya mawili ya Tangatanga na Kieleweke wanasema makundi hayo yanalenga kupanua demokrasia chamani.
Joshua Kutuny aliyekuwa rafiki wa karibu wa Ruto na mbunge wa Jubilee sasa amebadilika na kuwa mkosoaji wake mkubwa: "Imani imetuleta sisi watu wa Kieleweke pamoja, tulianza wachache - watu wanne, sasa tuko zaidi ya wabunge 60 ndani ya huu msafara. Hakuna siku rais amenambia kuwa haungi mkono. Wale wengine walianza wakiwa mia sasa naona wako saba."
Joto la siasa linazidi kufukuta miaka mitatu kabla ya uchaguzi mkuu!
Ruto ameyataka makundi hayo mawili kukoma kupiga siasa hadi wakati mwafaka utakapojiri. Ameukosoa upinzani kwa kusema kuwa hauna msingi wowote wa kukishauri chama chake kuhusu masuala ya maendeleo. Gathoni Muchomba ni mbunge maalum wa upande wa Tangatanga, na anadhani Jubilee kinapaswa kuwa mwakilishi wa taifa zima la Kenya: "Tumesikia wengine wameanza vyama vyao vya ukabila. Ili Jubilee ije pamoja, vyama 14 vilivunjwa ili kiwe chama cha kitaifa."
Licha ya kwamba bado miaka mitatu kwa Wakenya kushiriki kwenye uchaguzi mwingine, tayari joto la siasa linazidi kufukuta pembe zote za taifa, hali inayoibua suala la viongozi kutimiza ahadi zao kabla ya uchaguzi huo. Wanasiasa wanazunguka kote, kutafuta miungano na kura. Katika taifa ambalo vyama hutumika tu kama viunzi vya kumpitisha mtu kuwa kiongozi na baadaye vikazikwa, je chama tawala cha Jubilee kitayashinda mawimbi haya na kuibuka kidedea kwenye uchaguzi mkuu ujao ama kitakufa tu kama vyama vinavyokufa vyama vyengine na kusahaulika nchini Kenya?