1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano kuhusu mkataba wa hali ya hewa

19 Desemba 2009

Nchi zinazoendelea za G77 zimekataa kuukubali mkataba huo ambao sio wa kisheria lakini China imeuidhinisha.

https://p.dw.com/p/L8hZ
Mkataba wa hali ya hewa waidhinishwa na viongozi wachache wa nchi zenye nguvuPicha: AP

Viongozi wa nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya wamezungumzia kuvunjwa moyo na mkataba kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa uliofikiwa katika mkutano wa kilele wa Umoja wa mataifa mjini Copenhagen wakisema kwamba malengo yao ya kupunguza viwango vya utoaji wa gesi inayoharibu mazingira hayakulinganishwa na nchi zingine. Baadhi ya viongozi hao wanasema kwamba mkataba huo hauna maana yoyote na hasa baada ya nchi zinazoendelea kushindwa kukubaliana na mkataba huo katika suala la upunguzaji wa gesi chafu ya Carbon dioxide.

Kiongozi wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso amesema kwamba hatua ya kukosa kufikiwa makubaliana ya kisheria ni suala ambalo linazusha wasiwasi mkubwa. Pamoja na hayo amesema kwamba ni bora kufikiwa makubaliano kuliko kukosekana.

Bundeskanzlerin Angela Merkel Kopenhagen Klimagipfel Rede
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel asema ni Uamuzi mgumu uliopitishwa lakini hauna budiPicha: AP

Kwa upande mwingine kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema anayatazama matokeo ya mkutano huo kwa hisia tofauti akisema kwamba hatua mbadala ambayo ingechukuliwa katika mkutano huo ingelikuwa ni kutopatikana mwafaka wowote hali ambayo ingemaanisha kushindwa kwa kikao hicho.Aidha Kansela Markel amejitolea kuandaa mkutano mwingine wa kufuatailia kikao cha Copenhagen mnamo katikati ya mwaka 2010.

Amesema kwamba kinachohitajika kwa sasa ni kuona kwamba shirika la Umoja wa mataifa linalohusiana na mazingira linadhibiti utekelezaji wa hatua zilizofikiwa katika mkutano huo. Halikadhalika rais wa Ufarsana Nicolas Sarkozy amesema mkataba uliofikiwa ni hatua pekee ambayo ingeweza kufikiwa baada ya kujitokeza mgawanyiko mkubwa katika kikao hicho.

Sudan Dänemark Lumumba Stanislaus Di-Aping Sprecher der GZZ
Katikati ni,Lumumba Di-Aping kutoka Sudan, kiongozi wa kundi la G77 asema hawatosaini mkatabaPicha: AP

Mvutano umejitokeza hii leo miongoni mwa wajumbe walioko katika kikao hicho kuhusiana na mkataba huo uliofikiwa na kundi la viongozi wachache,nchi nyingi maskini zinasema kwamba mkataba huo unaongeza hali ya kukiukwa kwa Umoja wa Mataifa. Mwakilishi wa Venezuela amesema mkataba huo unadhihirisha wazi kupinduliwa kwa Umoja wa Mataifa na viongozi wa chache wa nchi zenye nguvu.

Nchi nyingi zinazoendelea katika kundi la G77 hadi sasa zimeukataa mkataba huo ambao zaidi umeonekana kupendekezwa na rais wa Marekani Barack Obama pamoja na viongozi wengine wa nchi zenye nguvu duniani.China lakini imewatupa mkono washirika wake wa kundi la G77 na badala yake imeuidhinisha mkataba huo.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri Grace Patricia Kabogo.