1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano kati ya Poland na Umoja wa Ulaya Magazetini

Oumilkheir Hamidou
24 Julai 2017

Mvutano kati ya serikali ya Poland na Umoja wa Ulaya, kitisho cha kuzuka wimbi jengine la machafuko kati ya Israel na wapalastina na jinsi suala la wakimbizi linavyotishia kugubika kampeni za uchaguzi magazetini

https://p.dw.com/p/2h3NS
Polen Protest gegen Justizreform in Warschau
Picha: Reuters/K. Pempel

Tunaanzia Poland ambako mbinu za chama tawala PiS za kutaka kudhibiti taasisi za sheria zimesababisha mvutano pamoja na Umoja wa Ulaya. Gazeti la Allgemeine Zeitung la mjini Mainz linaandika: "Msiba unapiga Poland na mwisho wake haujulikani. Chama tawala PiS kinajiandaa kuachana na mfumo wa demokrasia. Kwasababu hiyo ndio tafsiri ya  mipango ya kuuingilia mfumo wa sheria na vyombo vya habari. Na hasa Poland, nchi iliyokuwa kwa muda mrefu ikisifiwa kama ya kiliberali na mfano wa kuigizwa miongoni mwa nchi zilizojiunga na Umoja wa Ulaya. Na hasa Poland ambayo mapambano yake ya kuania uhuru mapema miaka ya 80 ndio yaliyofungua njia ya kuporomoka ukuta wa Berlin na kumalizika vita baridi.

Gazeti la kaskazini mwa Ujerumani,"Hannoversche Allgemeine" linahisi wananchi wengi wa Poland wanaamini neema iliyoko nchini inatokana na chama tawala cha PiS. Gazeti linaendelea kuandika: "Wapoland wengi wanakishukuria chama tawala cha PiS kwa kuzidisha sana ruzuku kwaajili ya watoto. Zaidi ya hayo wengi wanafurahia hali bora ya maisha inayozidi kunawiri. Ukweli lakini ni kwamba uchumi wa Poland unanawiri kwa kiasi hicho kwasababu ya soko la pamoja la Umoja wa ulaya. Lakini kuporomoka ukuta mwaka 1989 kuna faida gani ikiwa leo hii kila mmoja anajijengea ukuta wake?

Mzozo wa Haram Al Sharif

Habari za hivi punde zinasema rais wa Poland ameamua kutumia kura yake ya turufu kupinga mswaada wa mageuzi ya sheria uliopendekezwa na chama tawala cha PiS."Tukitoka ulaya tunaelekea Mashariki ya kati ambako daamu inaendelea kumwagika tangu Israel ilipoamua kuweka mkitambo ya chuma kuwakagua waumini wa kiislam wanaotaka kwenda kusali katika msikiti mtukufu wa Al Aqsa. Baraza la usalama la umoja wa mataifa linakutana leo kusaka njia za kutuliza hali ya mambo. Gazeti la "Badische Zeitung" linaandika:"

Hakuna mengi yanayotarajiwa badala ya miito kwa pande zote mbili zijizuwie. Wenye usemi utakaotuliza hali ya mambo wanakutikana huko huo, katika eneo la mzozo. Benjamin Netanyahu atalazimika kuregeza kamba akitaka kuzuwia moto usiendelee kuenea.

 Kampeni za Uchaguzi Ujerumani

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kampeni za uchaguzi nchini Ujerumani. Gazeti la "Der neu Tag" linaandika kuhusu mjadala uliozuka upya kuhusu mzozo wa waakimbizi. Gazeti linaendelea kuandika: "Martin Schulz ametamka lile neno ambalo hadi wakati huu lilikuwa marufuku. Miko katika kampeni za uchaguzi mkuu kuzungumzia mada tete kama hiyo. Na hasa kuhusu neno "mzozo wa wakimbizi". Kansela Angela Merkel analikwepa neno hilo tangu miezi kadhaa iliyopita. Hata mwenyekiti wa chama cha Christian Social Union CSU, Horst Seehofer ameliondowa angalao kwa sasa  katika ilani ya kampeni yao ya uchaguzi, suala analolipenda la "kikomo ".Lakini sasa limezushwa upya. Na wote watatu wanatambua fika wimbi la wahamiaji halitosita. Kufungwa njia ya Balkan na mkataba wa wakimbizi pamoja na Uturuki hayakuleta ufumbuzi wa maana, yameliweka kando tu tatizo hilo.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu