Mvua yasababisha mafuriko, Kenya.
3 Desemba 2019Familia hizo zilikimbilia maeneo salama kuepuka athari zaidi ya mafuriko ambayo tayari yamesababisha uharibifu mkubwa wa mali ikiwemo mimea shambani.
Takriban wakaazi wapatao 1,000 eneo la Nyando kaunti ya Kisumu wameachwa bila makao wakilazimika kuhamisha baadhi ya mali zao ili kukimbilia maeneo salama wakiyakimbia mafuriko ambayo yameingia hadi kwenye makaazi yao baada ya mvua nyingi inayoendelea kushuhudiwa eneo hili na maeneo mengine ya nchi.
"Kila mwaka tuko tu na shida ya mwaji, inajaa kwa nyumba inaenda na kila kitu" alisema Caroline.
Wakaazi akiwemo Mercy Adhiambo, wanasema kando na mimea, mifugo na mali nyinginezo zimesombwa, na wanahofia wapendwa wao waliozikwa katika siku za hivi karibuni maana, wamelazimika kuweka mawe kwenye makaburi ili kuzuia waliozikwa kusombwa.
"Juma lililopita tulikuwa na matanga hapa, baada ya siku nne hivi.” Alisema Mawe
Vijiji ambavyo vimeathirika pakubwa kutokana na mafuriko haya ni Kasiwindi Kusini, Kanyipola Kusini, Kasambura, Kalo Kaskazini na Kalo Kusini, huku waathiriwa wakipiga kambi katika shule ya kimsingi ya Masau. Chifu wa kijiji cha Ombaka- Kakola, Jacob Ong'udi alinukuliwa akisema, "Tupo na vijiji vinne ambavyo vimeathirika pakubwa, na maeneo mengine pia yamefurika na kwa sasa tumewahamisha waathiriwa hadi shule ya Masau ambako wamepiga kambi.” amesema Chifu Ong'udi.
Idadi hii ya wakaazi 1,000 walioathiriwa ni jumla ya kaya zaidi ya 150 katika hali inayojiri huku kupitia taarifa yake, idara ya utabiri wa hali ya anga nchini Kenya ikionya kuwa mvua nyingi ambayo inaendelea kushuhudiwa kote nchini huenda ikaendelea kwa siku kadhaa ikitaja maeneo yanayotazamiwa kushuhudia kiwango cha juu cha mvua kuwa Kusini na kati mwa Bonde la Ufa, Nyanza, Kusini na Kati mwa eneo la Kati, Nairobi na maeneo ya karibu.