1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvua kubwa yasababisha vifo vya watu 17 kaskazini mwa Sudan

Sylvia Mwehozi
7 Agosti 2024

Mvua kubwa iliyonyesha kaskazini mwa Sudan, imesababisha vifo vya watu 17 na majengo kuporomoka, wakati nchi hiyo ikikabiliwa na mapigano ya takriban miezi 16 kati ya vikosi pinzani.

https://p.dw.com/p/4jBbh
Mafuriko ya Sudan
Athari za mvua huko Sudan mwaka 2022Picha: Sami Alopap/AA/picture alliance

Mvua kubwa iliyonyesha kaskazini mwa Sudan, imesababisha vifo vya watu 17 na majengo kuporomoka, wakati nchi hiyo ikikabiliwa na mapigano ya takriban miezi 16 kati ya vikosi pinzani.

Waziri wa miundombinu wa jimbo hilo Samir Saad aliwaambia waandishi wa habari, kwamba nyumba zipatazo elfu 11,500 tayari zimebomoka na takriban watu 170 wamejeruhiwa.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni katika jimbo la Mto Nile lililoko karibu kilometa 400 kaskazini mwa mji mkuu wa Khartoum. Taarifa zinasema kuwa umeme umekatika na watu wanalala nje usiku kucha wakihofia mvua zaidi kunyesha.

Kila mwaka mtiririko wa maji kwenye Mto Nile huambatana na mvua kubwa zinazoharibu nyumba, miundombinu na kupoteza maisha. Athari zinatarajiwa kuwa mbaya zaidi mwaka huu kufuatia mapigano ambayo yamesababisha mamilioni ya watu kukimbilia maeneo ya mafuriko.