Muungano wa kijeshi wa Saudia waendelea kuishambulia Hodeida
14 Juni 2018Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulianzisha mashambulizi dhidi ya mji huo wa bandari hapo jana, na leo mapema asubuhi milio ya makombora imerejea tena kusikika. Bandari hiyo kwenye Bahari ya Sham ni muhimu sana kwa pande zote kwenye vita hivi, kwani ndilo lango la kuingizia chakula kwenye taifa hilo ambalo tayari limeshakumbwa na ukosefu mkubwa wa chakula.
Saudi Arabia na washirika wake wanataka kuwang'oa Wahouthi kutoka ngome yao hiyo wanayoishikilia tangu mwaka 2015. Lakini licha ya silaha nzito na za kisasa walizonazo Wasaudi na wenzao, wengi wanatabiri kwamba mapambano yatachukuwa muda mrefu na yenye madhara makubwa kutokana na Wahouthi kujichimbia kwenye mitaa ya mji huo.
"Idara zote za wizara za Mambo ya Ndani na Ulinzi zipo ndani ya mji na kila mahala. Vikosi vyetu viko makini tukiwafuatilia maadui zetu. Na watakapoamuwa kuingia, watatukuta sisi ni kama milima, hatung'oki," alisema Mujib Mohammed, kamanda kwenye jeshi la Kihouthi:
Wapiganaji wanaoungwa mkono na muungano wa Saudia wameonekana hadi sasa wakiwa kwenye viunga vya mji huo, ambako wamewaonesha waandishi wa habari kile wanachodai kuwa ni sheheha ya silaha zilizotengenezwa Iran na ambazo waliziteka kwenye mji wa pwani wa Al-Hima, uliowahi kuwa ngome ya Wahouthi.
Operesheni mbaya kabisa
Operesheni hii ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia inatajwa kuwa kubwa kabisa kuwahi kufanywa tangu ulipoivamia nchi hiyo kwa lengo la kuiondoa serikali inayoongozwa na Wahouthi wanaodaiwa kuungwa mkono na hasimu mkubwa wa Saudia, Iran.
Mashirika ya misaada yanahofia kwamba huenda bandari ya Hodeida ikalazimika kufungwa na hivyo kuzuwia uingiaji wa chakula, katika hali ambapo tayari nchi hiyo imekumbwa na baa la njaa, huku robo tatu ya raia milioni 27 wakitegemea chakula cha msaada. Takribani asilimia 70 ya chakula kinachoingizwa Yemen hupitia bandari hiyo.
Wakati mapigano yakiendelea, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kukutana kwenye kikao cha ndani hivi leo, kutokana na ombi la Uingereza, ili kujadili mashambulizi haya. Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Martin Griffiths, amesema umoja huo unazungumza na pande zote mbili kuzitaka ziwache mapigano.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman