Museveni, Magufuli kuimarisha biashara na ushirikiano
10 Novemba 2017Raia wa nchi zote mbili walipata fursa nadra ya kuvuka mpaka kati ya nchi hizo bila kufuata utaratibu ili kushuhudia makaribisho ya Rais Magufuli nchini Uganda ambapo miongoni mwa yaliyo kwenye ratiba yake ni kutembelea pia eneo ambako Uganda inajiandaa kuchimba mafuta.
Rais Magufuli ameelezea kuwa hiyo ndiyo hali inayostahili kwa mataifa ya Afrika kwani vizingiti kwenye mipaka yao ndiyo hupelekea maendeleo kukwama.
Uzinduzi wa kituo hicho ni mojawapo ya hatua za kurahisisha biashara na uhamiaji chini ya mchakato wa kutekeleza itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashiriki. Vituo vingine kama hivyo vimejengwa kwenye mipaka ya nchi hizo na Kenya pamoja na Rwanda.
Rais Museveni Museveni ametoa angalizo kuwa watu wan chi hizo mbili wanatakiwa kuwezeshwa kuendesha shughuli zao ili kuleta ufanisi kanda hiyo.
Marais hao walioandamana na wake zao ambao wote wanaitwa Janet walikariri kuwa ipo haja kuondoa urasimu unaosababisha shughuli za kiuchumi na kijamii kufanyika.
Wametoa mfano kuwa kituo cha Mutukula kimerahisisha usafirishaji wa chakula kutoka Tanzania hadi sudan kusini ambako shirika la mpango wa chakula duniani kinasambaza misaada hiyo kwa wakimbizi.
Tangu shughuli za kituo hicho kuanza mwaka 2015 nchi zote mbili zimepata makusanyo zaidi kuliko hapo awali kwani kimepunguza visa vya ulaji rushwa. Makusanyo kwa upande wa Uganda yameongezeka kwa asilimia 110.
Baada ya kuzindua kituo hicho, Rais Magufuli na mwenyeji wake walielekea sehemu ambako ujenzi wa bomba la mafuta utaanza kwa upande wa Uganda.
Tayari mradi huo umeanza kutekelezwa Tanga. Aidha rais magufuli atambelea pia maeneo ambako Uganda inajiandaa kuanza kuchimba mafuta ghafi.
Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala
Mhariri: Mohammed Khelef