1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni avikosoa vyombo vyake vya usalama kwa utesaji

Daniel Gakuba
17 Mei 2017

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amekosoa visa vya utesaji ambavyo vyombo vya usalama nchini mwake vinatuhumiwa kuvifanya, akisema vitendo hivyo sio sahihi na sio vya lazima.

https://p.dw.com/p/2d5tZ
Yoweri Museveni Präsident Uganda
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Hoshiko

Katika barua aliyowaandikia wakuu wa polisi na idara ya upelelezi, Museveni amesema maafisa wa usalama wanaweza kumfanyia mateso mtu asiyehusika kabisa na uhalifu, ambaye anaweza kukiri makosa ili aweze kujinusuru na mateso hayo, na kusisitiza kuwa hiyo si haki.

Hata hivyo kiongozi huyo amekosolewa na watetezi wa haki za binadamu kwa kutoanzisha uchunguzi kuhusu visa hivyo.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekuwa mara kwa mara likitaja kuwepo vitendo vya utesaji dhidi ya wafungwa nchini Uganda.

Kauli ya Museveni imefuatia kuibuka kwa picha zinazomuonesha meya wa mji wa Kamwenge Kusini Magharibi mwa Uganda, Geoffrey Byamukama, akiwa na majeraha ya kutisha mwilini, ambayo anasema yalisababishwa na vipigo vya polisi wakati akihojiwa kuhusiana na mauaji ya aliyekuwa msemaji wa polisi ya Uganda Andrew Kaweesi.