1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni aongoza kura za maoni Uganda

Emmanuel Lubega25 Januari 2016

Wiki chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Uganda wa tarehe 18 Februari, matokeo ya utafiti wa maoni yanaonesha kuwa mgombea wa chama tawala, Rais Yoweri Museveni, anaongoza kwa asilimia zaidi ya 70.

https://p.dw.com/p/1HjUo
Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda.Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Gazeti linaloegemea upande wa serikali la New Vision liliwasilisha matokeo ya utafiti wa kura ya maoni kuhusu nafasi za wagombea urais na kwa mujibu wa matokeo hayo, Rais Museveni anaweza kushinda kwa asilimia 71 ya kura akifuatwa kwa mbali na mpinzani wake wa siku nyingi, Dk. Kizza Besigye, kwa asilimia 19 tu. Amama Mbabazi ambaye alitazamiwa kuwavutia baadhi ya wafuasi wa chama tawala NRM ambako alikuwa katibu mkuu yumo katika nafasi ya tatu kwa asilimia 6 tu.

Lakini wakosoaji wa utafiti huo wanasema gazeti hilo linatumiwa na utawala wa Rais Museveni kuwashawishi wapigaji kura kwamba wapende wasipende jenerali huyo wa kijeshi, ambaye ametawala kwa takribani miaka 30 sasa, angali kipenzi cha wengi.

Siku moja baada ya kuchapishwa kwa matokeo hayo, nalo shirika la Research World International lilitoa matokeo ya utafiti wake uliofanywa kati ya tarehe 19 Desemba 2015 hadi tarehe 10 Januari 2016, ambayo yanaonesha Rais Museveni anaongoza kwa asilimia 51 akifuatwa na Dk. Besigye kwa asilimia 32 huku Mbabazi akibashiriwa kupata asilimia 12 ya kura. Ofono Opondo, msemaji wa chama cha Museveni, NRM, alisema hata kama bado mgombea wake angali anaongoza na hivyo hakuna matarajio ya duru ya pili ya uchaguzi, lakini "sikubaliani na kauli kwamba umaarufu wake umeshuka kutoka asilimia 73."

Tofauti kati ya matokeo ya New Vision na yale ya Research World International yanaupa upinzani taswira kwamba wana uwezo wa kumkosesha Rais Museveni ushindi wa moja kwa moja wakiondoa asilimia mbili hivi kutoka kwa matokeo hayo na hivyo kusababisha duru ya pili ya uchaguzi ambapo kinyang'anyiro kitakuwa kati ya mshindi na anayemfuata.

Matokeo mengine ya utafiti huo wa kura ya maoni ni kwamba kuna vuta-nikuvute kati ya wale wanaotaka mabadiliko ya utawala na wale ambao wanamtaka Rais Museveni aendelee kuongoza Uganda. Tofauti kati ya wanaotaka na wasiotaka mabadiliko ni aslimia tatu tu. Aidha wengi wanataka kumchagua kiongozi ambaye si tu ana ujuzi bali pia aliye na sera na mawazo mapya.

Kulingana na tathimini zote mbili, Rais Museveni angali kipenzi cha wengi kutokana na mafanikio ya uongozi wake kuendeleza amani, usalama na uthabiti wa kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kinachopelekea chuki dhidi ya utawala wake ni kushamiri kwa ufisadi na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira.

Suala lingine ambalo lilichunguzwa ni hofu walizonazo wananchi kuhusiana na uchaguzi mkuu huo utakaofanyika tarehe 18 Februari. Asilimia 44 ya watu waliohojiwa walielezea kwamba huenda msukosuko wa kisiasa ukatokea huku asilimia 27 wakielezea mashaka ya udanganyifu kutokea katika uchaguzi huo.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala
Mhariri: Iddi Ssessanga