MUSCAT : Maelfu waandamana dhidi ya vifungo kwa Waislamu wa siasa kali
4 Mei 2005Maelfu ya wananchi wa Oman wameandamana hapo jana dhidi ya kufungwa kwa Waislamu wa siasa kali 31 waliopatikana na hatia ya kula njama ya kulipinduwa taifa hilo la Ghuba la Arabuni linalounga mkono mataifa ya magharibi.
Mwanaharakati wa haki za binaadamu Abdullah Al Riyami ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba polisi iliingia kwa nguvu kwenye uwa wa msikiti mmoja katika mji mkuu wa Muscat ambapo waandamanaji hao walikuwa wamekusanyika na kuwapiga marungu katika jaribio la kuwatawanya.Pia amesema kwamba watu kadhaa wametiwa mbaroni.
Mahkama nchini Oman hapo jana iliwahukumu watu sita kifungo cha miaka 20 gerezani wakati wengine 24 wamehukumiwa vifungo vya miaka 7 hadi 10 na mmoja amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja.
Watu hao pia wameonekana na hatia ya kuunda kundi la siri kinyume na sheria kupanga kuipindua serikali ya Mfalme Qaboos kwa kutumia nguvu,kumiliki na kuuza silaha na kufanya mikutano ya kuwaorodhesha wanachama.
Serikali inawashutumu watu hao kwa kujaribu kuunda utawala wa Masheikh wa Kiislam nchini Oman.