1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Munich ina miadi jumapili hii na Hamburg

22 Februari 2008

Munich yaionya Hamburg kujiandaa barabara kesho ama sivyo itanyolewa na wembe uliowanyoa Hannover mwishoni mwa juma liliopita.

https://p.dw.com/p/DBvJ
Miroslav Klose (B.Munich)Picha: AP

Viongozi wa Bundesliga-Bayern Munich wanakumbana jumapili na Hamburg wakijua wana kibarua kigumu cha kupanda mlima.

Chelsea ikijua Arsenal london imefungua mwanya wa pointi 5 mbele ya Mancheste united,imepania kutwaa kesho taji lake la kwanza katika finali ya Kombe la FA na Birmingham.

Mwanamichezo wetu eric Ponda anatusimulia ilikuaje Tusker FC ikawaachia Al Tahrira kutoroka na ushindi hata bila kubidi kuteremka uwanjani mjini Nairobi na kwanini FIFA imewatimua nje wajumbe 3 wa chama cha mpira cha Kenya.

Ni ramadhan ali tena nikishirikiana na Alex Mwakideu katika michezo wiki hii:

BUNDESLIGA:

Tukianza na Bundesliga-Ligi ya ujerumani-viongozi wa Ligi hiyo bayern Munich wana matumaini makubwa kutamba mbele ya Hamburg kufuatia ushindi wao wa mabao 5-1 juzi dhidi ya Aberdeen katika kombe la ulaya la UEFA.Isitoshe, mwishoni mwa wiki iliopita,jogoo lao la itali-Luca Toni lilitamba katika lango la Hannover lilipotia mabao 3 pekee.

Isitoshe, Munich haitamtegemea luca toni pekee kesho,kwani jogoo lake jengine chipukizi Lukas podolski limepona na juzi alikomea mabao 2 pekee katika lango la Aberdeen ya scotland kukamilisha ushindi wa mabao 5-1 la waskochi wa Aberdeen.

Kinyume na Munich, hamburg haikutamba juzi katika kombe la UEFA na ilikata tiketi yake ya duru ijayo ya kombe hili kwa kumudu sare tu 0:0 na FC zurich ya uswisi.Hii lakini litosha kuwapa ushindi wa mabao 3:1 kutokana na duru zote mbili.

Shaka-shaka kwa Bayern munich iliofungua mwanya wa pointi 3 kileleni kati yake na Werder Bremen ni iwapo jogoo lake jengine la kati ya uwanja mfaransa Franck Ribbery nalo limepona.

Katika Serie A-ligi ya itali ,Inter Milan haikufungwa hata mara moja tangu kuanza msimu huu na imefungua mwanya wa pointi 11 kilelelni ikiandamwa na AS roma.Lakini juzi katika champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya, Inter ilikiona cha mtema kuni.Liverpool ikitamba nyumbani iliizaba Inter mabao 2-0.Kesho Inter inaitembelea Sampdoria .Mlinzi wake Marco Materazzi ,ambae utakumbuka ndie alieopigwa dafurau katika finali ya kombe la dunia na Zinedine Zidane wa Ufaransa, alitolewa nje ya uwanja na rifu jumane iliopita huko Uingereza baada ya kadi 2 za manjano.Na pale Zlatan Ibrahimovic allipoulizwa Inter imekumbwa na msiba gani, alijibu „kamuulizeni Metarazzi“.

Katika Premier League-Ligi ya Uingereza, Manchester united na Arsenal London zinarudia uhasama wao katika kinyan’ganyiro cha premier League-Ligi ya Uingereza.Arsenal inaongoza Ligi hii kwa pointi 5 ikifuatwa na Manchester United .Macho ya mashabiki wa dimba lakini watayakodoa huko Birmingham kesho,kwani huko,

FINALI YA KOMBE LA LIGI YA FA HUKO UINGEREZA:

Kesho ni finali ya kombe la FA uwanjani wembley,U ingereza.Chelsea –the Blues- wanateremka uwanjani kutetea taji lao la ubingwa wa kombe hilo kati yao na Totten Hotspurs.Chelsea inaania vikombe 4 msimu huu na kesho inapanga kutia kapuni kombe lao la kwanza.Wanatapia kombe la ubingwa wa uingereza, kombe la Ulaya la klabu bingwa ,premier League na kombe la FA.

Wenzao Tottenham wako katika duru ijayo ya kombe la ulaya la UEFA baada ya kuirarua Slavia-Prague ya jamhuri ya Czech kwa mabao 3-2.Ushindi kesho utawavalisha taji lao la kwsanza tangu 1999 walipotoroka na kombe hilo.

Tangu enzi hizo, maadui zao kesho-Chelsea wamekwisha twaa ubingwa wa Uingereza mara 2 ,kombe la chama cha mpira cha Uingereza FA na tena Kombe la ligi la FA.Pia msimu uliopita ,chelsea ilitamba mbele ya Arsenal.

Chelsea walishinda finali ya mwaka jana ya kombe hili huko Cardiff, wanaingia uwanjani Wembley kesho wakipigiwa upatu kombe ni lao.Kwani, Chelsea msimu huu wameshindwa mechi 3 katika mapambano 41 ya vikombe mbali mbali.Isitoshe hawakushindwa katika mapambano 16 yaliopita tangu walipozabwa bao 1:0 na Arsenal desemba mwaka uliopita.

Wachezaji wake mashuhuri na hatari kama Muivory Coast Didier drogba na mghana Michael Essien wamesharudi kutoka Kombe la afrika la mataifa ili kuimarisha Chelsea wakati nahodha wao John Terry na mchezaji wao wa kiungo Frank Lampard wameshapona kutoka maumivu waliopata.

Chelsea imeshacheza mara 2 katika uwanja huu mpya wa wembley ilipoikumta Manchester united katika finali ya kombe la FA mwezi Mei uliopita na kutoka nao sare katika kuania ngao ya Community shield August mwaka jana.

Spurs wamerudi katika jukwa la dimba wakiwa na nguvu zaidi wakati huu kuliko msimu huu ulipoanza.Wako sasa imara tangu kinguvu hata kimawazo.

Na ushahidi wa hayo ni ushindi wao wa kishindo wa mabao 5-1 dhidi ya viongozi wa Ligi Arsenal katika duru ya pili ya nusu-finali ya kombe hili.Lakini, licha ya kulazwa katika mapambano 5 kati ya 27 chini ya kocha Ramos,wangali hawakuifikia hadhi ya Chelsea.

Kwahivyo, kesho asie na mwana aeleke jiwe-mkutano uwanjani Wembley,kwani kwa Tottenham Hotspur-kesho ni kufa-kupona.kwa Chelsea wao wameshakata tiketi ya champions League na wana matumaini ya kuweza kutamba huko.

Mwishoni mwa wiki iliopita, duru ya kwanza ya mkuania kombe la klabu bingwa barani Afrika ilianza huku zamalek ya Misri,ikiania kufuata nyayo za timu ya taifa kutwaa kombe la afrika ilianza uzuri huko Kigali Rwanda ilipoitoa APR kwa mabao 2:0.

Mwishoe, michezo ijayo ya Olimpik ambayo bila ya wanariadha wa Kenya itakuwa bila ya wali bila mchuzi:

Kwa upande wa Uingereza, kamati yake ya Olimpik inapanga kuandaa kambi ya mazowezi kabla michezo hiyo-pre-Olympic training camp huko Macau-koloni la zamani la Mreno nchini China.kikosi cha wanariadha wake 250 kikijumuisha makocha,wanariadha 131 watakaoshiriki katika michezo 15 mbali mbali na maafisa kadhaa kitafanya mazowezi yake huko Macau kwa wiki 2-3 kabla michezo kufunguliwa rasmi August 8.mwaka huu.

Uingereza inaegemeza matumaini yake ya medali ya dhahabu mara hii tena kwa bingwa wakewa mbio za marathon za wanawake- Paula Radcliffe na muingereza wa asili ya Nigeria –bingwa wa dunia wa mita 400 Christine Ohurougu, lakini pia mbondia Frankie Gavin na Beth Tweddle stadi wa gymnastics.