Mume wa mwanariadha wa Kenya Agnes Tirop akamatwa na polisi
15 Oktoba 2021Ibrahim Rotich ambaye ndiye mshukiwa mkuu wa mauaji ya Agnes Tirop alikamatwa mwendo wa saa tatu Alhamisi usiku mjini Mombasa kwa mujibu wa vyombo vya usalama. Gari lake jeupe la Toyota NZE, lilikuwa limebondeka, polisi wakisema kuwa alisababisha ajali walipokuwa wakimfukuza. Mshukiwa anahojiwa na atashtakiwa kwa makosa ya mauaji.
Rotich alikamatwa siku moja tu baada ya Tirop, mshindi wa dunia mara mbili wa nishani za shaba kupatikana ameuawa kwa kudungwa nyumbani kwake Iten, katika eneo la bonde la ufa, kilomita 800 kutoka Mombasa. Mwili wa Tirop mwenye umri wa miaka 25, ulipatikana kwenye dimbwi la damu na majeraha ya kiuno nyumbani kwake, Iten. Kamanda wa Polisi katika kituo cha Changamwe David Mathiu anafafanua.
"Uchunguzi bado unaendelea na kama mnavyojua sisi tunafuata sheria, mshukiwa atapelekwa kortni, kuhusiana na mauaji ya mkimbiaji shupavu, Agnes Chebet Tirop.”,alisema Mathiu
Soma pia:Mshindi wa medali ya mashindano ya dunia Kenya Tirop afariki
Polisi walimtambua Rotich kuwa mshukiwa mkuu na mara moja wakaanzisha uchunguzi. Inasemekana kuwa baada ya mshukiwa kutekeleza unyama huo, alipigia familia ya marehemu simu akikiri makosa yake.
Rotich alikamatwa na mtu mwengine ambaye walikuwa wanasafiri pamoja. Aidha simu ya marehemu ilipatikana kwenye gari la mshukiwa huyo. Tom Makori ni Afisa Mkuu wa Polisi katika eneo la Keiyo Kaskazini, mahali Agnes Tirop alipopatikana ameuawa.
"Bwana alikuwa amepigia wazazi simu akilia, akiwaeleza kuwa, Mungu amsamehe, kuna kitu amefanya, hiyo ilifanya polisi kuenda kuangalia nyumba ya Tirop.”
Soma pia:Biden aahidi msaada zaidi wa chanjo ya corona kwa Afrika
''Ni mumewe aliyemuua''
Inasemekana kuwa Rotich na Tirop walikuwa wameoana kwa njia ya kitamaduni, lakini walikuwa wameachana. Familia zao zilijaribu kuwapatanisha na walikuwa wameishi kwa juma moja kabla ya mkasa kutokea. Hata hivyo mamake marehemu Dinah Tirop, amekanusha madai hayo.
"Hatujawahi kumuona, hata vile watu walivyokuwa wakisema mitandaoni, ni mumewe aliyemuua, hatujawahi sikia na hajawahi kuja nyumbani na hatujapeana msichana.”
Agnes Tirop alikuwa ameanza kuogelea kwenye kizingiti cha ufanisi baada ya kushinda mbio za masafa marefu ya dunia mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 19 tu. Aidha alishinda nishani za shaba katika mbio za mita 10,000 mwaka 2017 na 2019 katika mashindano ya riadha ya dunia. Alimaliza wa nne katika mashindano ya olimpiki ya mita 5000 yaliyokamalika majuzi jijini Tokyo, Japan.
Mwezi uliopita alivunja rekodi katika mashindano ya riadha ya kina dada ya kilomita 10. Wakenya wanapoendelea kuomboleza kwa kuondokewa kwa nyota wao, ni bayana kuwa ivumayo haidumu.