1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe atimia miaka 83, akisisitiza bado yupo madarakani

Mohamed Abdul Ra´hman21 Februari 2007

Awaambia wanaowania kiti chake, kwa sasa hakuna nafasi, bali ataondoka wakati ukiwadia.

https://p.dw.com/p/CHJf
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe
Rais Robert Mugabe wa ZimbabwePicha: AP

Kiongozi mkongwe barani Afrika Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, leo ametimiza miaka 83 ya kuzaliwa, huku akisisitiza tena kwamba bado hakuna nafasi ya kazi ya Urais, akiwaonya wale wenye kiu cha nafasi hiyo miongoni mwa mawaziri wake kusitisha harakati za kuiwania.

Katika hotuba yake iliotangazwa na televisheni ya taifa na vituo vinne vya matangazo ya redio nchini humo Rais Mugabe alisema utafika wakati ataondoka madarakani lakini bado. Huku akiongeza kwamba wanaolijadili suala hilo wanaweza kuendelea kufanya hivyo, lakini badala yake kinachomshangaza ni baadhi ya watu kuanza kuranda huku na kule huku wakijiuliza watajaza nafasi gani, kwani hata kama hawajifikirii kuwa ni wao watakaojaza nafasi ya Urais ,lakini wanajiuliza watakua katika nafasi gani.

Mugabe yuko madarakani tangu 1980 wakati nchi hiyo ilipojipatia uhuru kutoka kwa Uingereza, lakini baada ya miaka 27 madarakani, anakabiliwa na matatizo ya kisiasa na kiuchumi, wakati ughali wa maisha ukitajwa kupanda hadi 1,600 asili mia. Uhaba wa chakula jambo ambalo halikua likisikika hapo kabla, sasa umezagaa kote nchini na 80 asili mia ya wakaazi wanaishi katika hali ya umasikini.

Rais Mugabe alishadokeza hapo awali kwamba atastaafu baada ya kipindi chake kuamalizika mwaka ujao 2008, lakini wafuasi wake katika chama tawala ZANU-PF wamepitisha azimio la chama kumrefushia muda kwa miaka miwili zaidi hadi 2010 wakati utakapofanyika pia uchaguzi wa bunge. Na inatarajiwa kwamba bunge linalodhibitiwa na ZANU-PF, litaidhinisha hatua hiyo ya kumrefushia kipindi chake cha utawala. Kamati mkuu ya chama tawala itakutana kuidhinisha hatua hiyo mwezi ujao.

Chama kikuu cha upinzani Movement for Democratic change-MDC kinasema kitaendelea na maandalizi yake na shinikizo la dhidi ya Mugambe kikizingatia kwamba muda wake unamalizika mwaka ujao.

Suala la nani atamrithi Mugabe linaonekana kusababisha mgawanyiko katika chama hicho, kati ya wanaomuunga mkono Makamu wa rais Joyce Mujuru na wale wanaoiunga mkono kambi ya Waziri wa makaazi vijijini Emmerson Munangagwa.

Wakati akiadhimisha mwaka wa 83 wa kuzaliwa, Mugabe amewashambulia mawaziri wake akisema wengi hawaaminiki na wamejiingiza katika visa vya Rushwa. Aidha hakuacha kumshambulia pia hasimu yake mkubwa-waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair, akimshutumu kuwa anakula njama na Rais George W. Bush wa Marekani kwa madai yasio na ukweli, wakiwa na malengo ya kutaka Zimbabwe iekewe vikwazo vya kiuchumi.

Alisema Zimbabwe haikuwakosea Wamarekani, lakini kinachomuuma Bw Blair ni sera ya mageuzi nchini Zimbabwe ambalo ni suala la wazimbabwe wenyewe.