1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe amsimamisha kazi mwanasheria mkuu

15 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Cc7Q

HARARE.Rais Robert Mugabe amesimamisha kazi mwanasheria mkuu wa serikali na kuunda tume ya watu watatu kuchunguza shutuma ya kwamba mwanasheria huyo alitumia vibaya madaraka yake.

Sobusa Gula-Ndebele alikamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa uzembe katika kesi ya mfanyakazi wa benki aliyetoroka tarehe 8 mwezi uliyopita, lakini baadaye aliachiwa na kuendelea na kazi.

Taarifa iliyotolewa na katibu wa baraza la mawaziri nchini Zimbabwe, Misheck Sibanda imesema kuwa mwanasheria mkuu huyo amesimamishwa kazi kuanzia jana.

Uamuzi huo unakuja siku moja tu baada ya hapo jana chama kinachotawala nchini Zimbabwe kumpitisha Rais Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 83 kama mgombea pekee wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani.