Mugabe amekufa lakini masaibu ya Zimbabwe yanaendelea
7 Septemba 2019Ulikuwa usiku wa joto Oktoba 2009, mimi na viongozi wenzangu wa wanafunzi tulikuwa kwenye usaifiri wa umma kuelekea nyumbani baada ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wa mwenzetu. Akilini mwetu, safari hiyo ilikuwa ya kukamilisha kile kilichokuwa siku ya furaha. Hakuna kati yetu alijua kuwa matukio hayo yangechukuwa mwelekeo usiotarajiwa na tungeishia jela.
Baada ya kupanda basi dogo la abiria kwenye uwanja wa soko, mmoja ya vituo vyenye shughuli nyingi zaidi katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, kuelekea kitongoji cha watu wa tabaka la chini cha Glen View, tuliungana na abiria wenzetu katika mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ya kila siku.
Nchini Zimbabwe ambako nafasi ya haki za binadamu ilikuwa finyu, watu mara nyingi hujiepusha kushiriki mijadala ya umma kuhusu siasa na kasoro za serikali. Mazungumzo hayo yalikuwa ya hisia na uchangamfu. Abiria walielezea kwa uwazi na kwa hisia juu ya kutoridhika kwao na kuendelea kudorora kwa hali ya kiuchumi na ukandamizaji wa kikatili dhidi ya aina yoyote ya upinzani.
Robert Mugabe, akiwa bado rais wakati huo, alikuwa anakataa mpango wa kuunda serikali shirikishi kufuatia kushindwa kwake katika uchaguzi wa rais na kiongozi wa upinzani wakati huo Morgan Tsvangirai, ambaye alifariki baadae kwa ugonjwa wa saratani mnao 2018. Mmoja ya wenzangu alizungumza kwa sauti juu ya namna Mugabe alivyokuwa chanzo cha mgogoro wa kisiasa wa Zimbabwe, kutokana na kuendelea kudhoofisha pande zilizokuwa ziunde serikali.
Baadhi ya abiria wenzetu walipiga kelele kwamba kutajwa tu kwa Mugabe kunaweza kumuweka matatani kila mmoja aliekuwepo kwenye basi hilo. Kuthibitisha maneno hayo, dereva aligeuza ghafla na kuliendesha basi hilo kuelekea kituo kikuu cha polisi cha Harare.
Baada ya kufika kituoni hapo, maarufu kwa kuwa kitovu cha ufungwaji kiholela, askari polisi wanne wenye silaha walioarifiwa kuhusu kilichojiri hawakupoteza muda na wakatutia pingu huku wakitutangazia kwamba tumetenda kosa la "uhaini." Kwa muda wa masaa mawili, tulihojiwa na kupigwa vibaya kabla ya kuwekwa kwenye vyumba vichafu vya jela.
Baadhi ya marafiki zangu walikuwa wakivuja damu, lakini walinyimwa huduma za matibabu. Kilichofuatia kilikuwa siku mbili za kukaa katika kizuwizi cha polisi hadi tulipoachiwa.
Mapinduzi yaliosalitiwa
Hili lilikuwa mmojawapo ya matukio mengi niliyokumbana nayo kama mwanaharakati mwanafunzi chini ya miaka ya kuogofya ya utawala wa Mugabe. Kutukana au kudharau ofisi ya rais lilikuwa mojawapo ya makosa ya kawaidi yanayotumiwa kuwashtaki Wazimbabwe kwa kutekeleza uhuru wao wa kujieleza uliodhaminiwa kwenye katiba.
Nilikuwa mojawapo ya wanaharakati wanafunzi waliokamatwa, kupigwa, kufungwa na kuondolewa madarasani wakati wa utawala wa Mugabe. Baada ya kuundwa mwaka 1999 kwa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change MDC, ambamo vuguvugu la wanafunzi lilikuwa na mchango mkubwa, ukandamizaji wa Mugabe dhidi ya wanaharakati wanafunzi ukazidi kuwa mbaya.
Kwa kuweka rekodi, wanafunzi walikufa, baadhi walipigwa marufuku kusoma nchini Zimbabwe maisha yao yote, baadhi walisimamishwa masomo, na yote hayo yalikuwa mojawapo tu ya silaha ambazo Mugabe alizitumia kuwanyamazisha wakosoaji wakubwa: wanafunzi.
Tulihisi kualitiwa na Mugabe na kizazi chake kutokana na ubinafsi na uroho wao, ambavyo viliwanyima vijana wa Zimbabwe fursa ya kushiriki matunda ya ukombozi wa Zimbabwe. Kuporomoka kwa uchumi, ukosefu wa ajira, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka vilinipa hamasa ya kupinga utawala wake, ingawa hiyo ilikuwa njia hatari kuifuata kutokana na matukio ya kutoweka, mashambulizi na kukamatwa vilivyopripotiwa kila siku.
Washiriki wengi bado wapo
Baada ya kutangazwa kwa kifo cha Mugabe siku ya Ijumaa, nilitafakari juu ya urithi wake. Mwanaume ambaye, katika miaka yake ya kwanza madarakani, aliongoza sera kali ya elimu kwa wote, na kwa juhudi zake hizo, raia wengi wa Zimbabwe kutoka familia maskini walinufaika. Ndoto ya elimu kwa wote kufikia mwaka 2000 iligeuka zimwi wakati Mugabe alipobinafsisha na kuigeuza elimu kuwa bidhaa, na kusababisha maelfu ya wanafunzi kutoka familia maskini kukosa elimu ya juu.
Wakati urithi wa Mugabe ukiendelea kujadiliwa, itakuwa busara kwetu kuuliza iwapo alikuwa pekee yake katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliougubika utawala wake na kuuporomosha uchumi wa Zimbabwe. Jibu ni hapana. Mugabe hakuwa peke yake: Aliwakilisha mfumo wa serikali ninaouita "Mugabeism."
Kupinduliwa kwake mwaka 2017 na kifo chake wiki hii vimedhihirisha nguvu nyuma ya miaka yake 37 ya kuogoya. Rekodi ya Zimbabwe kuhusu uvunjaji wa haki za binadamu inaendela na inazidi kuwa mbaya chini ya viongozi wanaojaribu kujitenga naye. Mwisho wa yote, Robert Mugabe alifariki akiwa mtu mwenye uchungu, baada ya kusalitiwa na maluteni wake aliowaamini.