1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Mugabe aachia watu wapigwe na Afrika yakodowa macho"

Ute Schaeffer/Oummilkheir14 Machi 2007

Hali nchini ZImbabwe baada ya maandamano ya amani ya jumapili iliyopita

https://p.dw.com/p/CB5G
Morgan Tsvangirai anasemekana amejeruhiwa vibaya sana kichwani
Morgan Tsvangirai anasemekana amejeruhiwa vibaya sana kichwaniPicha: AP

Zinatisha!-hivyo tuu ndivyo mtu anavyoweza kuzitaja picha za kiongozi wa upande wa upinzani nchini Zimbabwe,Morgan Tsvangirai.

Alipokua njiani kuelekea mahakamani jana,alikua kama mtu aliyezubaa,amenyolewa nywele upande mmoja kwasababu ya majaraha kichwani na macho yake yamevimba.Ameteswa alipokua akishikiliwa na polisi mjini Harare. ”

Robert Mugabe ni mfano halisi wa muimla.Kutoka mpigania uhuru mwenye bashasha na shujaa wa Afrika,amegeuka hivi sasa muimla anaewakandamiza na kuwateka nyara wakaazi wote wa Zimbabwe.Mugabe, ambae akiwa kiongozi wa wanamgambo aliutimua madarakani utawala wa kikoloni wa wazungu wachache,anafanya yale yale maovu -tawala wa mabavu,na ubaguzi,ya sera za ukoloni dhidi ya nchi yake.

Anapenda kuchochea hisia za chuki dhidi ya wakoloni ili kujiimarisha madarakani.Heshi kuikaripia siasa ya “wazungu” na hasa waengereza na wamarekani,anaowatwika jukumu la kuiangamiza nchi yake.

Lakini wasisingizwe wengine bure.Hakuna,isipokua yeye mwenyewe Robert Mugabe,aliyeigeuza fakhari ya Afrika kua mahala pa ufukara.Anaitawala Zimbabwe tangu uhuru mwaka 1980.Ni siasa yake ya uzembe iliyosababisha kuporomoka Zimbabwe kiuchumi na na kujikuta ikitengwa kisiasa.

Mugabe amesahau kabisa kwamba siasa imelengwa kuwatumikia wananchi na kudhamini pia mahitaji yao ya kimsingi.

Hii leo ughali wa maisha nchini Zimbabwe umefikia kiwango cha juu kuliko nchi yoyote ile nyengine ulimwenguni-asili mia 1700!Asili mia 80 ya wananchi wa Zimbabwe hawana kazi.Kuna ukosefu wa mafuta,nyama, na mkate na huduma za umeme zinakurubia kusita.Mavuno ya mahindi kwa mwaka huu yanatazamiwa kufikia nusu tuu ya kiwango kinachohitajika.Katika nchi tajiri kwa nafaka barani Afrika,watu wanakumbwa na njaa.

Mugabe amegeuka kitambulisho cha waliofeli barani Afrika.Cha kusikitisha ni kwamba ,baada ya uhuru,nchi hiyo ilikua na kila uwezo, sawa na Afrika kusini, kufanikiwa kisiasa na kiuchumi.Mitindo ya kupendeleana na rushwa ndiyo inayodumisha utawala wa Mugabe-hawajali hata kidogo hatima ya wananchi walio wengi ,wasiojimudu.Mugabe amewapokonya ardhi maelfu ya mabwana shamba wakizungu-ameigawa kwa wale wanaomnyenyekea-wakulima walio wengi wanajukita hawana kazi.Makadirio ya wastani ya maisha kwa wakinamama,hayapindukii miaka 34.

Hadi wakati huu wazimbabwe wamekua wakivumilia.Hawamjui rais mwengine.Hofu na woga umeenea kila pembe,ndio maana watu hawasubutu kufanya chochote.Na Mugabe ameshasema ataendelea,hata baada ya uchaguzi wa mwaka 2008.Akifanya hivyo basi nchi hiyo itapotelewa na kila kiumbe kinachoweza kukimbia.

Kukamatwa na kuteswa kiongozi wa upande wa upinzani Morgan Tsvangirai na wanaharakati wengineo wanaodai mageuzi kunaweza kukomesha hali hiyo.Na lawama kutoka nje na ndani,toka serikali yake mwenyewe Robert Mugabe zinazidi kusikika.Lakini kwamba wazimbabwe wajikwamue kutoka hofu na hali ya kukata tama na kujikomboa toka makucha ya muimla,hakuna anaeamini,hasa baada ya miongo mitatu ya utawala wa kimabavu na vitisho.

Pengine kinachoweza kubadilisha hali ya mambo ni shinikizo linalozidi kukua kutoka chama chake mwenyewe Mugabe.

Nchi za nje zinabidi pia ziwajibike.Cha kuhuzunisha ni jinsi nchi jirani zilivyonyamaza kimya;na hasa Afrika kusini na Umoja wa Afrika.