1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muda wayoyoma kuinusuru Pembe ya Afrika

Josephat Charo
20 Mei 2022

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwamba muda unayoyoma kulinusuru eneo la pembe ya Afrika kutokana na ukame na kuyaokoa maisha ya raia. Umoja huo umetoa wito msaada wa fedha utolewe haraka kulisaidia eneo hilo

https://p.dw.com/p/4BdDe
Martin Griffiths
Martin GriffithsPicha: UN/Mark Garten

Mratibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia utoaji wa misaada ya dharura Martin Griffiths ameuambia mkutano wa waandishi habari mjini Geneva kwamba muda unawatupa mkono na wanahitaji fedha kwa haraka sana kuokoa maisha. Griffiths alikuwa akizungumza, siku mbili baada ya kufanya ziara nchini Kenya.

Umoja wa Mataifa umesema eneo la Pembe ya Afrika linakabiliwa na ukame mbaya kabisa katika historia yake, huku watu zaidi ya milioni 15 wakikabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa usalama wa upatikanaji chakula na uhaba mkubwa wa maji kote nchini Ethiopia, Kenya na Somalia. Idadi hiyo huenda ikafikia watu milioni 20 iwapo mvua chache chini ya kiwango zinatorarajiwa hazitanyesha.

Griffiths aidha alisema hali huenda ikazidi kuwa mbaya kwa watu wengi zaidi katika wiki zijazo huku hali ya msimu wa mvua kuanzia mwezi wa Oktoba hadi Desemba ikitarajiwa kuwa mbaya kama ilivyokuwa katika misimu minne iliyopita. Amesema hali hiyo inatishia sio tu uhai wa watu bali pia mfumo wao mzima wa maisha.

Umoja wa Mataifa unasema kote nchini Kenya, Somalia na Ethiopia, takriban watoto milioni 5.7 wanakabiliwa na utapiamlo mkali, huku mifungo zaidi ya milioni tatu wanaotegemewa na familia za wafugaji kwa kujipatia kipato, wakiwa wamekufa. Griffiths amesema watu kulazimika kuyahama maeneo yao ndilo suala kubwa lililojitokeza sana katika mazungumzo yake nchini Kenya. Aliongeza kusema uhamaji kutokana na ukame umedhibitiwa kwa kiasi katika maeneo yenye ukame, ikilinganishwa na uhamaji kutokana na mizozo.

Nepal Wirtschaft Junelo
Picha: Rebecca Conway/Getty Images

Hali ni mbaya Ethiopia

Kamishna huyo wa Umoja wa Mataifa amesema Ethiopiainakabiliwa na changamoto ya ukame na mzozo na ikiwa mapigano katika eneo la kaskazini yataendelea kuchacha na kuenea, basi pana haja ya kuwa na hofu kuhusu wimbi la watu kukimbia na kuvuka mipaka ya nchi. Ameongeza kusema eneo la Pembe ya Afrika halitengewi fedha za kutosha, na fedha zinazowekezwa huko ni fedha ambazo zingesaidia kwa kuwa mateso ni makubwa mno yasiyo mithili.

Katika eneo la Sahel nako hali ni kama hiyo. Amesema watu hadi milioni 18 katika ukanda huo watakabiliwa na uhaba wa chakula katika kipindi cha miezi mitatu ijayo. Shirika la kutoa misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa lilizindua kampeni yake ya kukusanya fedha ya mwaka 2022 mwezi Desemba mwaka uliopita, likitaka dola bilioni 41 kusaidia watu milioni 274 wanaohitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi. Lakini sasa linahitaji dola bilioni 46 kuwasaidia watu milioni 303, huku likitaka kuwafikia milioni 202 kati ya hao.

Griffiths amesema wafadhili mpaka sasa wamechanga karibu dola bilioni sita, kiwango ambacho ni cha juu na kimeweka rekodi kutolewa kufikia wakati huu wa mwaka. Lakini ametahadharisha kwamba kwa kuwa ufadhili kwa ajili ya misaada ya kiutu umeongezeka hadi kufikia bilioni 19 kwa mwaka na bajeti ya mwaka huu imeongezeka, hawatafanikiwa kufikia hata nusu yake.

afp