Muda wa makubaliano wa Iran wasogezwa mbele
7 Julai 2015Taarifa ya kurefushwa mazungumzo hayo ilitolewa na Marekani licha ya kuwa leo ndio siku ya mwisho iliyopangwa makubaliano kamili kufikiwa.
Msemaji mkuu wa ujumbe wa Marekani Marie Harf amesema mazungumzo hayo yamepiga hatua lakini pia ni mazungumzo yenye uzito mkubwa kwa pande zote mbili. Ameongeza kuwa wanajali zaidi ubora wa mpango wa makubaliano kuliko muda watakaochukuwa kufikia makubaliano.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema atabaki katika mazungumzo hayo kwa siku kadhaa zijazo pamoja na pande zote husika ili kuhahkikisha makubaliano yanafikiwa.
"Tutaendelea na mazungumzo kwa siku kadhaa zijazo. Hii haimanishi kuwat unarefusha muda wa mwisho wa kufikiwa makubaliano ya kudumu. Makubaliano ya kudumu yana uwezekano wa kupatikana ingawa sasa tunakabiliana na kipindi kigumu cha maamuzi," alisema Federica Mogerini.
Naye waziri wa nchi za nje wa urusi Sergei Lavrov amesema kuiondolea Iran vikwazo vya silaha ilivyoekewa ndio tatizo kikubwa zaidi katika mazungumzo hayo kuweza kufikiwa makubaliano, huku Iran kwa upande wake ikitaka vikwazo hivyo viondolewe.
Hata hivyo ripoti iliyotolewa na Marekani baada ya mkutano uliopita mwezi Aprili baina ya pande hizo mbili, imesema vikwazo hivyo vitabaki kuwepo hadi mkataba wa mwisho utakapofikiwa
Wsiwasi wa nchi za magharibi
Maafisa wa nchi za magharibi wanawasiwasi kuiruhusu Iran kununuwa silaha kutoka nje kutachochea mzozo unaoendelea mashariki ya kati. Iran hata hivyo pia inasaidia katika jitihada za Marekani za kupambana na wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS nchini Iraq.
Mazungumzo hayo yanayoendelea ya mpango wa nyuklia baina ya Iran na nchi sita - Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani yanalenga kupunguza kasi mpango wa Iran wa nishati ya nyuklia kwa zaidi ya muongo mmoja ujao, na badala yake Iran itaondolewa vikwazo ilivyowekewa ambavyo vimeuathiri usafirishaji wa mafuta wa nchi hiyo pamoja na uchumi mzima kwa jumla.
Hii ni mara ya tano tangu mwaka 2013 kwa pande hizo mbili kushindwa kufikia makubaliano kamili katika muda uliopangwa. Katika mazungumzo ya hivi karibuni siku ya mwisho ya kufikiwa makubaliano ilikuwa ni Juni 30, muda ambao ulisogezwa mbele hadi leo Julai 7, na sasa umepelekwa tena mbele hadi Ijumaa ijayo, Julai 10.
Mwandishi: Yusra Buwayhid
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman