Muda wa kusitisha mapigano Homs waongezwa kwa siku tatu
13 Februari 2014Gavana wa Homs Talal al Barazi amesema mapigano yatasitishwa katika mji huo kwa siku tatu nyingine kuanzia leo ili kuruhusu raia zaidi kuondoka na kuongeza kuwa jumla ya watu 1,4000 wameondolewa tangu Ijumaa iliyopita wakati makubaliano yalipofikiwa kati ya pande mbili zinazozana.
Hata hivyo wanaume wa kati ya umri wa miaka 18 hadi 55 wapatao 300 ambao wanaaminika ni wa umri na wenye nguvu za kubeba silaha na kushiriki katika vita wamekuwa wakizuiwa na majeshi ya serikali kuhojiwa.
Uingereza na Marekani zashutumu kuzuiwa kwa wanaume
Barazi amesema 70 kati yao wameachiwa huru hii leo.Uingereza imeshutumu hatua hiyo ya kuwazuia wanaume na kusema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuwa makini zaidi ili utawala wa Rais Bashar al Assad usitumie kisingizio cha kuruhusu raia kuondoka Homs kuendeleza mateso na mauaji zaidi mjini humo
Taarifa kutoka wizara ya mambo ya nje ya Marekani pia imesema serikali ya Syria imeahidi kuwaachia wanaume hao baada ya kuwachunguza na inataraji itatimiza ahadi hiyo na kuongeza inafuatilia kwa karibu hatima ya wanaume hao.
Wakati huo huo, mpatanishi mkuu wa Umoja wa Mataifa na nchi za kiarabu Lakhdhar Brahimi anatarajiwa kukutana na wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Urusi na Marekani mjini Geneva hii leo ili kujaribu kufufua matumaini ya kupatikana ufumbuzi wa mzozo huo wa Syria kupitia mazungumzo ya amani ambayo yanaonekana kukwama.
Urusi kuushinikiza utawala wa Syria
Barhimi anatarajiwa kukutana na naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Gennady Gatilov na katibu mwandamizi wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Wendy Sherman ili kuyakwamua mazungumzo hayo.
Baada ya siku tatu za vuta nikuvute kati ya wajumbe wa serikali na wa upande wa waasi kuhusu nani wa kulaumiwa kwa vita hivyo vya Syria,pande hizo mbili leo hazikupangiwa kuwa na mikutano.
Mazungumzo hayo yaliyoanza tarehe 22 mwezi Januari yaliandaliwa kwa pamoja na Marekani na Urusi.Huku yakionekana kukwama,Urusi ambayo ni mshirika wa utawala wa Syria inatarajiwa kuishinikiza serikali ya Assad kusongesha mbele mchakato huo wa kutafuta amani.
Huku duru hiyo ya pili ya mazungumzo inayotarajiwa kukamilika Jumamosi hii ikionekana kutofua dafu,mapigano ambayo yanaripotiwa kupamaba moto katika mji wa Aleppo yamewaua kiasi ya watu 51 wakiwemo waasi 13.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Syria lenye makao yake Uingereza limesema wengi wa waathiriwa waliuawa kupitia mashambulizi ya angani yaliyofanywa na wanajeshi wa serikali.
Na Meli ya kijeshi ya Marekani imetia inapangiwa kutia nanga nchini Uhispania leo ikisubiri serikali ya Syria kuikabidhi silaha za sumu ili zikaharibiwe baharini.Taarifa kutoka ubalozi wa Marekani Uhispania imesema meli hiyo ijulikanayo MV Cape Ray itazisafirisha silaha hizo za sumu kuambatana na maagizo ya umoja wa Mataifa hadi katika bandari ya Italia zitakakopakuliwa.
Mwandishi:Caro Robi/afp/reuters/ap
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman