1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muda wa kusimamisha mapigano Gaza waongezwa

14 Agosti 2014

Mpango wa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza kwa siku nyingine tano, umeanza kutekelezwa leo (14.08.2014) na unaendelea kuheshimiwa.

https://p.dw.com/p/1CueS
Mahmoud Abbas akiwa na Benjamin Netanyahu
Mahmoud Abbas akiwa na Benjamin NetanyahuPicha: CHRIS KLEPONIS/AFP/Getty Images

Mpango huo umefikiwa baada ya Israel na Hamas kukubaliana kuongeza muda wa mazungumzo yanayosimamiwa na Misri ya kujaribu kumaliza vita vya Gaza. Hata hivyo, muda huo umeanza kwa mashaka, baada ya jeshi la Israel kusema kuwa wapiganaji wa Gaza wamekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano baada ya kufyatua maroketi manane kwenye eneo la Israel, hatua iliyoifanya nchi hiyo nayo kulipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi ya anga katika maeneo ya magaidi.

Afisa wa Hamas, Izzat Reshiq amekanusha taarifa kwamba Palestina imekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na imeyalaani vikali mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel kama ukiukaji wa hali ya utulivu. Hata hivyo hakuna taarifa zozote za kuwepo waathirika wa mashambulizi hayo.

Moja ya maeneo ya Gaza yaliyoharibiwa na mapigano
Moja ya maeneo ya Gaza yaliyoharibiwa na mapiganoPicha: DW/Bettina Marx

Muda wa saa 72 uliotangazwa kwa mara ya pili, wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza, ulimalizika usiku wa jana Jumatano, lakini dakika za mwisho, Palestina ikatangaza mjini Cairo, kuongeza makubaliano hayo kwa siku tano zaidi, ili pande zote ziweze kuendelea na mazungumzo ya kumaliza vita, yanayosimamiwa na Misri.

Muda sasa kuwa wa saa 120

Kiongozi wa ujumbe wa Fatah katika mazungumzo hayo, Azzam Ahmed, amesema badala ya saa 72 sasa itakuwa saa 120 na kwamba ujumbe wa Palestina utaondoka kwenda Ramallah kwa mazungumzo na Rais Mahmoud Abbas na uongozi wa Kipalestina.

Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, afisa wa Israel amesema nchi yake imeukubali muda huo ulioongezwa. Hata hivyo inaonekana kuwa tofauti zilizopo kati ya Israel na Palestina katika suala la kutafuta amani ya kudumu ni gumu kutatuliwa. Hamas na washirika wake wanataka kuondolewa kabisa kwa hatua ya kuzingirwa ukanda huo na Israel na Misri.

Viongozi wa makundi ya Palestina wakiwa mjini Cairo
Viongozi wa makundi ya Palestina wakiwa mjini CairoPicha: Khaled Desouki/AFP/Getty Images

Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh, jana amekiambia kituo cha televisheni cha Hamas cha Al-Aqsa kwamba kundi hilo linasisitiza kuondolewa kwa hatua ya kuzingirwa. Duru za Misri na Palestina zinaeleza kuwa Israel imekubali kuruhusu baadhi ya bidhaa kuingia Gaza.

Mapigano kati ya Israel na Palestina, yaliyodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja yamesababisha Wapalestina 1,945 na Waisraeli 67 kuuwawa na maelfu wengine kuachwa bila makaazi. Mapigano hayo yamesababisha vifo vingi zaidi, tangu pande hizo mbili zilipopigana vita kwa muda wa wiki tatu mnamo mwaka 2008 na 2009, wakati wa majira ya baridi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE
Mhariri: Iddi Ssessanga