Muafaka wa kusitisha mapigano Gaza magazetini
22 Novemba 2012Kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, gazeti la Stuttgarter Nachrichten linasema ari ya Misri kujitwika jukumu la upatinishi linaonekana limezaa matunda na huenda likawa na umuhimu mkubwa katika siku zijazo na katika makubaliano haya ya kusitishwa kwa mapigano.
Mhariri wa gazeti hilo anasema kama Israel inataka kuendelea kuuzingira Ukanda wa Gaza na kukidhibiti kikamilifu kitisho kipya cha makundi ya wanamgambo wa kiislamu katika eneo la Misri la Sinai, basi inahitaji ushirikiano kutoka kwa upande wa serikali ya Misri mjini Cairo. Kundi la Hamas halishirikiani sana kwa karibu na Misri katika kuishawishi Israel ilegeze kamba msimamo wake wa kuuzingira Ukanda wa Gaza.
Msimamo huo wa Hamas hata hivyo kwa muda mrefu hauisumbui tena Misri katika jitihada zake za kuzirudisha pande hizo mbili zinazozozana, katika mkondo wa mazungumzo ya amani. Misri imeonyesha japo kwa kiwango kidogo, uwezo wake wa kutuliza mzozo huo. Lakini swali la muhimu zaidi ni nani atakayeweza kuchukua jukumu hili la upatanishi, kwani kwa sasa hapaonekani mtu wa kufanya hivyo!
Kitisho cha harakati ya ardhini
Nalo gazeti la Wiesbadener Kurier kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati linasema waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, hadi sasa ameshikilia msimamo wake wa upande mmoja - harakati ya kijeshi dhidi ya Gaza kama mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza hayatakoma.
Mhariri anatilia maanani kwamba kama Netanyahu ataendelea kuukumbatia msimamo huu, basi licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa na jududi zote za kimataifa za kutafuta suluhu, Israel itafanya harakati ya kijeshi ya ardhini katika kipindi kifupi au kirefu kijacho.
Juhudi za kuisaidia Ugiriki
Mada nyingine iliyozingatiwa na wahariri leo ni juhudi za kuisaidia Ugiriki kifedha ili isifilisike. Gazeti la Lausitzer Rundschau linasema waokoaji wa nchi hiyo wanalazimika sasa kuwa wakweli.
Mhariri anasema kama vile Ujerumani ilivyolazimika na kujenga umoja wa kuhamisha fedha na nchi mpya za Umoja wa Ulaya, ndivyo Umoja huo unavyotakiwa kufanya pia na Ugiriki. Kwani umoja wa sarafu katika Umoja wa Umoja wa Ulaya unajumisha kuhamisha fedha kutoka nchi moja hadi nyingine.
Baadaye hatua hii itatakikana kuchukuliwa pia na Ureno. Kwa sababu nchi hizi mbili, tofauti kabisa na Uhispania na Italia, kwa muda mrefu hazitaweza kujisimamia zenyewe katika masuala ya fedha. Kwa sasa hazihitaji mpango wa kubana matumizi - lazima zisaidiwe kifedha, hata na fedha za walipa kodi wa Ujerumani.
Mwandishi: Josephat Charo/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman