Mtuhumiwa wa ujasusi aungama Marekani
2 Julai 2010Kwa mujibu wa waendesha mashtaka wa Marekani, mtuhumiwa huyo alikiri kuwa anaiamini zaidi serikali ya Urusi kuliko mwanawe wa kiume. Hata hivyo, Rais Medvedev wa Urusi bado hajatoa kauli yoyote kuhusiana na kisa hicho, ijapokuwa Waziri Mkuu, Vladmir Putin, aliyekuwa afisa wa ujasusi wa zamani katika Idara ya KGB, amevikosoa vyombo vya sheria vya Marekani. Kisa hicho kinahofiwa kuwa huenda kikauathiri uhusiano wa kidiplomasia kati ya Urusi na Marekani.
Jina la kughushi
Mtuhumiwa huyo aliyetumia jina lisilokuwa la kweli la Juan Lazaro, alieleza wazi kuwa mkewe, Vicky Palaez, ambaye ni mwandishi aliyezaliwa nchini Peru, alifanya safari kadhaa kuelekea Amerika ya Kusini kwa minajili ya kuwafichulia siri za kijasusi maafisa wa Urusi. Wawili hao ni sehemu ya watuhumiwa 11 waliohusika kwa njia moja au nyingine katika sakata la kuzifichua siri za kijasusi kati ya Marekani na Urusi. Jambo hilo linahofiwa kuwa litaziathiri juhudi za kuuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Tisa kati yao wanaisubiri hatima yao baada ya kuyawasilisha maombi ya kuachiwa kwa dhamana katika mahakama tatu tofauti. Wengine watano, wanaousibiri uamuzi wa kisheria katika miji ya Boston na Virginia, wamelazimika kurejea tena mahakamani baada ya kesi yao kuahirishwa ili kuipa nafasi ya kuutathmini ushahidi zaidi.
Barua ya Lazaro
Mkuu wa sheria wa mahakama ya jimbo la kusini la New York, Preet Bharara, aliielezea barua ya Lazaro ya kuungama aliyoandikiwa Jaji Ronald Ellis. Kulingana na barua hiyo, Lazaro alimuomba mwanasheria huyo kutofanya kosa kama lile lililotokea Cyprus ambako mtuhumiwa mmoja muhimu aliachiwa kwa dhamana na baada ya hapo alitoweka.
Katika taarifa yake ya kina aliyoielezea baada ya kuthibitisha kuwa anazikanusha haki zake kama mhalifu, kwa kufuata misingi ya katiba-maarufu onyo la Miranda- Lazaro alikiri kuwa hakuwa raia wa Uruaguay na kwamba Juan Lazaro si jina lake la kweli. Hata hivyo, kamwe hakujitambulisha kikamilifu. Alifafanua kuwa ijapokuwa anampenda sana mwanawe wa kiume, kamwe hatoukiuka wajibu wake kwa idara ya ujasusi ya Urusi, SVR, iliyozinduliwa baada ya ile ya KGB ya wakati wa utawala wa Kisovieti kuvunjwa.
Kwa upande wake, Jaji Ellis alisema kuwa atautangaza uamuzi wake baadaye, ila mkewe Lazaro,Vicky Pelaez,ataachiwa kwa dhamana ya kiasi cha dola laki mbili na nusu, na atazuiliwa nyumbani. Hiyo ni kwa sababu Vicky Pelaez si jasusi na ana jina la kweli na anafahimika kuwa ni raia wa Marekani aliye na haki ya kuishi katika nchi yoyote ile.
Maombi ya kuachiwa kwa dhamana
Yote hayo yakiendelea, Jaji Ellis alilitupilia mbali ombi la kuachiwa kwa dhamana watu wengine wawili, Richard na Cynthia Murphy, wanaotuhumiwa kutafuta mawasiliano na maafisa wa ngazi za juu tangu miaka ya tisaini walipojifanya kuwa wakaazi wa New Jersey.
Barua hiyohiyo aliyoandikiwa Bharara ilieleza pia kuwa shirika la ujasusi la Marekani, FBI, ilifanikiwa kufichua maandishi ya siri ambayo mpaka sasa hayajatangaziwa umma. Maafisa hao kadhalika walizipata barua 8 ambazo hazikuwa na maelezo zilikuwamo kiasi cha dola alfu kumi kumi za noti za dola mia.
Kwa upande mwengine, ombi la mtuhumiwa wa kumi, Anna Chapman, la kuachiwa kwa dhamana lilitupiliwa mbali. Kwa mujibu wa taarifa ya mume wake wa zamani Alex Chapman,iliyochapishwa hii leo. kwenye gazeti la Uingereza la Daily Telegraph, wawili hao walikutana mwaka 2001 katika hafla moja mjini London.Kabla ya kuolewa aliitwa Anna Kushchenko.
Mume wake huyo wa zamani, Alex Chapman,alisema kuwa hakushangazwa na madai hayo ya kuhusika na kashfa hiyo ya kijasusi kwani Anna alishamdokezea kuwa babake alikuwa na nafasi ya ngazi za juu katika shirika la ujasusi la zamani la Urusi, KGB. Alidai kwamba alikuwa jasusi wakati wa utawala wa Kisovieti nchini Urusi. Alex Chapman alieleza kuwa baada ya ndoa yao kusambaratika mwaka 2005,alihofia kuwa Anna alikuwa anaandaliwa kuwa jasusi. Kwa sasa Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza inayachunguza madai hayo.
Mafichoni Cyprus
Mtuhumiwa wa 11 Christopher Metsos alikamatwa Cyprus ila akatoweka baada ya kuachiwa kwa dhamana ya kiasi cha zaidi ya dola alfu 30 vilevile kuikabidhi mahakama hati yake ya kusafiri.Inahofiwa kuwa Metsos huenda akaelekea kwenye eneo la kaskazini la kisiwa hicho kilicho karibu na bahari ya Mediterana,ambako hakuna sheria zozote za kimataifa za kuwarejesha kwao watuhumiwa.Ifahamike kuwa eneo hilo linatumiwa sana kama maficho.
Katika kundi hilo ,watuhumiwa 9 huenda wakahukumiwa kifungo chahadi miaka 25 jela kwa mashtaka ya ulanguzi wa fedha pamoja na miaka mitano ya ziada kwa kukubali kushirikiana na serikali ya kigeni.Chapman na mmoja mwengine huenda wakakabiliwa na mashtaka mepesi zaidi.Ifahamike kuwa hakuna yeyote kati yao anayekabiliwa na mashtaka makali ya ujasusi.
Mwandishi:Thelma Mwadzaya –AFPE
Mhariri: Miraji Othman