1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtuhumiwa mauaji Marekani atoroka jela Kenya

8 Februari 2024

Mtu aliyekuwa akisubiri kupelekwa Marekani kufuatia waranti wa kukamatwa kwa madai ya kumuuwa mpenzi wake na kuuwacha mwili wake ndani ya gari kwenye uwanja wa ndege wa Boston ametoroka kizuizini nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/4cAj8
Polisi wa Kenya wakiwa kazini.
Polisi wa Kenya wakiwa kazini.Picha: THOMAS MUKOYA/REUTERS

Mkuu wa polisi jijini Nairobi, Adamson Bungei, alisema Kevin Adam Kinyanjui Kangethe alitoroka katika kituo cha polisi na kuingia katika gari ndogo la kibinafsi na kwamba polisi ilikuwa inafanya operesheni ya kumsaka.

Polisi wanne waliokuwa zamuni katika kituo hicho walitiwa mbaroni na wameandikisha taarifa kuhusiana na tukio hilo.

Maafisa hao walisema kuwa mwendo wa saa 10:00 jioni ya Jumatano (Februari 7), mtu aliyejitambulisha kama John Maina Ndegwa aliwaambia polisi hao kuwa yeye ni wakili wa Kangethe na akasema alitaka kumuona.

Kangethe aliondolewa kwenye seli yake na kisha yeye na Ndegwa wakaachwa kwenye ofisi, lakini muda mfupi baadaye, mtuhumiwa huyo alitoroka na kumuwacha wakili wake, ambaye amewekwa kizuizini.