Mtu mmoja auawa Bahrain
14 Februari 2013Mauaji ya kijana huyo, mwenye umri wa miaka 16, yametokea mapema leo katika kijiji cha Diah kilichopo magharibi mwa mji mkuu, Manama wakati maandamano hayo yalipogeuka kuwa ghasia kutokana na askari polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji. Watu walioshuhudia wamesema watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika ghasia hizo.
Upinzani umesema kijana aliyeuawa ametambuliwa kama Hussein al-Jaziri na kwamba amefariki kutokana na majeraha makubwa tumboni aliyoyapata baada ya kupigwa risasi na majeshi ya usalama. Upinzani nchini Bahrain umeitisha maandamano ya nchi nzima leo na kesho Ijumaa kuadhimisha miaka miwili ya vuguvugu la mageuzi lililoanza Februari 14 mwaka 2011, ambalo lilianzishwa na Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Mkuu wa usalama aonya
Mkuu wa usalama wa umma nchini Bahrain, Meja Jenerali Tariq al-Hassan alionya jana kuwa wale watakaojihusisha katika vitendo vyovyote visivyo halali watashughulikiwa ipasavyo. Hata hivyo, waandamanaji walipuuzia onyo hilo na kuingia mitaani katika vijiji vya Barbar, Bilad al-Qadim pamoja na Sitra na walizuia njia zote kuu za taifa hilo la Ghuba ambalo ni mshirika wa Marekani.
Jana usiku upinzani ulifanya mazungumzo ya maridhiano na serikali na wafuasi wake, ingawa bado hakuna dalili ya kufikiwa kwa muafaka. Mazungumzo hayo yamepongezwa na Marekani kama hatua moja mbele inayoweza kuleta mageuzi yatakayokidhi mahitaji ya watu wote wa Bahrain. Upinzani ambao unataka katiba ya kifalme, umedai kwamba matokeo ya mazungumzo hayo yawekwe kwenye kura ya maoni na sio kuwasilishwa kwa Mfalme Hamad bin Isa al-Khalifa kwa ajili ya kuidhinishwa.
Mazungumzo yazaa matunda
Mwakilishi wa upinzani katika mazungumzo hayo, Sayed Jameel Khadim, amesema makubaliano yamefikiwa katika mazungumzo ya jana na kwamba serikali iwe kama mdau mkuu katika mazungumzo hayo na matokeo yake yawekwe kwenye rasimu ya katiba. Wizara ya mambo ya ndani imesema kuwa awamu nyingine ya mazungumzo iliyokuwa ifanyike siku ya Jumapili, imefanyika jana kutokana na ombi la upinzani.
Makundi ya upinzani, likiwemo lile la Al-Wefaq, yaliamua dakika za mwisho kushiriki kwenye mazungumzo hayo baada ya kuyasusia mazungumzo ya kwanza ya Julai mwaka 2011, kwa madai kwamba hayakupewa uzito. Bahrain imekuwa katika mkwamo wa kisiasa tangu Februari mwaka 2011, huku serikali ikikataa kufikiwa kwa makubaliano ya kisiasa. Shirika la kimataifa la haki za binaadamu limesema kiasi watu 80 wameuawa tangu kuanza kwa vuguvugu hilo la kudai mageuzi ya kidemokrasia dhidi ya utawala wa kifalme unaoongozwa na Waislamu wa madhehebu ya Sunni.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri: Josephat Charo