1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waulaya wanapojaribu kufikiria kwa ujasiri zaidi

2 Novemba 2018

Uchaguzi wa bunge wa katikati ya muhula nchini Marekani haujawahi kufuatiliwa na watu nje ya nchi hiyo kama wa safari hii. Watu wengi barani Ulaya wanatumai matokeo ya uchaguzi huo yatazikata mbawa za rais Donald Trump.

https://p.dw.com/p/37aKp
Donald Trump spricht über Einwanderungspolitik
Picha: picture-alliance/C. Kleponis

Jarida la Ujerumani limewashangaza wasomaji wake kwa kuchapisha makala ya ziada juu ya uchunguzi wa maoni kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge wa katikati ya muhula nchini Marekani. Uchunguzi umebainisha jinsi wajerumani wanavyoufuatilia uchaguzi huo kwa kina kirefu.

Wajerumani,sawa na watu wengine katika nchi nyingine za Ulaya wanataka kujua iwapo matokeo ya uchaguzi huo yataleta mabadiliko katika sera ya nje ya rais Trump, ikiwa wagombea wa upinzani wa chama cha Demokratik watashinda uchaguzi huo. Watu wengi barani Ulaya wanataka wabunge wa chama cha Demokratik wapate viti vingi ili waweze kuuanzisha mchakato wa kumwondoa madarakani rais Trump . 

Jumanne ijayo wabunge kwenye wilaya 435 za majimbo yote 50 ya Marekani watachaguliwa upya. Kwenye baraza la seneti, theluthi moja ya wajumbe pia watachaguliwa upya.Mpaka sasa wajumbe wa chama cha Republican cha rais Donald Trump wanadhibiti matawi yote mawili ya bunge la Marekani.

Katika historia ya Marekani

Katika historia ya Marekani, chama cha upinzani huimarika wakati wa uchaguzi wa katikati ya muhula wa rais. Hayo pia ni maoni ya mtaalamu wa chama cha CDU wa masuala ya siasa barani Ulaya Elmar Brok ambae pia ni mshirika wa ndani wa Kansela Angela Merkel. Bwana Brok ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya masuala ya nje kwenye bunge la Ulaya amesema itakuwa vizuri endapo wajumbe wa chama cha Demokratik watadhibiti tawi mojawapo la bunge,baraza la wawakilishi au baraza la seneti.

Hata hivyo mtaalamu huyo ametahadharisha kwamba,ikiwa wajumbe wa chama cha demokratik watadhibiti tawi moja wapo na hivyo kuweza kumzuia Trump kutekeleza ajenda zake za mageuzi ya ndani, huenda rais huyo akaelekeza nguvu zake zote katika sera ya nje, jambo ambalo litasababisha wasiwasi mkubwa zaidi miongoni mwa watu barani Ulaya.

Na hata sasa watu barani Ulaya, wana wasi wasi mkubwa kutokana na mzozo wa kibiashara na Marekani. Sera ya biashara ya Trump imeshasababisha mvutano mkubwa na nchi za viwanda takriban zote duniani.  Trump ametishia kuyawekea ushuru magari kutoka nchi za Umoja wa Ulaya, baada ya kuzitosha ushuru bidhaa za chuma na bati. Trump amechukua hatua hiyo ili kuzilinda bidhaa za Marekani ndani ya nchi hiyo.

Ujerumani inaweza kuathirika sana.

Hata hivyo wataalamu wa Ujerumani wa masuala ya Marekani wanatahadharisha kwamba, hata  ikiwa wajumbe wa chama cha Demokratik watashinda uchaguzi huo,haina maana kuwa suluhu itapatikana  haraka katika vita vya kibiashara baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya.

Mtaalamu wa masuala ya Marekani, Josef Braml amesema hatarajii kuona mabadiliko katika sera ya biashara ya Marekani.Amesema wademokrats pia wana mtazamo mkali. Kwa kifupi, wanasema wataalamu wa Ulaya wa masuala ya Marekani, kwamba vyovyote itakavyotokea juu ya uchaguzi huo, watu barani Ulaya hawapwasi kuwa na matumaini makubwa ya kuona mabadiliko.

Wataalamu hao wanasema baada ya uchaguzi huo wa katikati ya muhula wa rais,Jumanne ijayo nchini Marekani mengi yanaweza kutokea. Jawabu ni moja.Umoja wa Ulaya unapaswwa kuwa na mkakati wa kuuwezesha kusimama yenyewe imara  katika siasa  za dunia.

Mwandishi: Zainab Aziz/Trippe, Christian/LINK: http://www.dw.com/a-46085996

Mhariri:Yusuf Saumu