1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Mtambue Dinknesh

25 Julai 2018

Bonde kuu la ufa ni nyumbani kwa mababu wa wanadamu. Dinknesh na wengine kama wao ni wa kwanza kutembea kwa kuinuka yaani kwa miguu miwili. Lakini bado waliishi kwenye miti.

https://p.dw.com/p/2rJMn

Dinkesh aligunduliwa wapi? Aligunduliwa karibu na kijiji cha Hadar nchini Ethiopia katika eneo la Afar ambalo ni sehemu ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki.

Kwanini Dinknesh amekuwa maarufu? Dinknesh huenda akawa aliishi miaka milioni 3.2 iliyopita. Wakati mifupa yake ilipochimbuliwa 1974, alitajwa kuwa ni mwanadamu wa kale aliyeishi duniani kuwahi kugunduliwa mabaki yake. Wanasayanysi wamegundua asilimia 40 ya mifupa hiyo, na kuyafanya kuwa mabaki ya kwanza ya binadamu wa kale yaliyo kamili zaidi. Dinknesh alitajwa kuwa ni aina mpya ya spishi iliyopewa jina la kisayansi la Australopithecus afarensis lenye maana ya 'sokwe wa kusini kutoka Afar'. Kwa kumsoma Dinknesh, wanasayansi walijifunza mengi kuhusu mabadiliko ya binaadamu. 

African Roots Lucy Dinknesh
Picha: Comic Republic

Lakini Dinknesh alikuwa sokwe ama? Hapana, Dinknesh hakuwa sokwe. Anafanana zaidi na binaadamu wa sasa kuliko sokwe. Na tayari alikuwa na maumbile ya kibinadamu. Utafiti kuhusu mabaki ya mifupa yake unaonyesha kwamba Lucy alikuwa anaweza kutembea ardhini kwa miguu yake miwili - ingawa inasemekana kuwa alipendelea zaidi kuishi juu ya miti kuliko ardhini.

Dinknesh alikuwa na umri gani? Kwa tathmini ya meno yake, mabaki ya mifupa yake ya mwili na ya uti wa mgongo, wanasayanyi wanaamini Dinknesh alikuwa na umri mdogo, lakini alifariki dunia wakati akiwa tayari mtu mzima.

Vipi alipewa majina ya Dinknesh na Lucy? Donald Johanson na Tom Gray, wanasayansi wa Kimarekani waliogundua mifupa ya Dinknesh, walisheherekea ugunduzi wao huo kwa kusikiliza wimbo wa kundi la Beatles uitwao "Lucy in the Sky with Diamonds". Hivyo ndivyo alivyolipata jina lake la kwanza la, Lucy. Jina lake lengine jipya zaidi ni Dinknesh, linalomaanisha 'wewe ni wa ajabu!' kwa lugha ya Kiamharik. Lakini jina la Lucy ndiyo maarufu zaidi. Anajulikana kama Dinknesh nchini Ethiopia pekee.


Ugunduzi wa kiekolojia wa hivi karibuni umenifanya nichanganyikiwe. Je Lucy amepoteza maana yake? Historia ya wanadamu daima itabaki kuwa na siri zisizojulikana. Uhusiano kati ya watangulizi wa binadamu na binadamu wa sasa utabaki kuwa suala lenye mvutano. Katika miaka ya karibuni, mbali na ugunduzi huo wa Lucy wa Ethiopia, ugunduzi mwengine wa spishi mpya wa Afrika Kuisni ulileta gumzo: Visukuku vya binadamu vilivyopewa jina la Homo naledi vinakadiriwa kuwa ni mabaki ya mifupa ya jamii ya binadamu walioishi miaka milioni 2.8 iliyopita -  miaka elfu kadhaa baada ya kuishi Dinknesh. Lakini bado kuna mjadala mkubwa kuhusu kukubaliwa kama moja ya jamii za binadamu zinazojulikana kisayansi kama homonini - jamii tofauti za binadamu wa kale ambao majina yao ya kisayansi huanzia na neno homo. Je chimbuko la homo sapiens, ambaye ni binadamu wa sasa ni: Morrocco? Ethiopia? Au pengine hata nje ya bara la Afrika? Hata hivyo, matokeo ya utafiti wowote mpya yanathibitisha kuwa watangulizi wa wanadamu wa kisasa, walikuwa Waafrika.

DW Videostill Projekt African Roots | Dinknesh, Lucy, Äthiopien
Picha: Comic Republic

Kuna mahala naweza kwenda kumuona Dinknesh? Ndio na hapana. Visukuku vya mabaki ya mifupa ya Dinknesh vimefichwa katika sehemu maalum iliyo salama katika Makumbusho ya Taifa ya Ethiopia iliyopo mji mkuu wa nchi hiyo, Addi Ababa. Lakini unaweza kumuona Dinknesh wa bandia aliyeigizwa maumbile ya Dinknesh katika makumbusho hiyo ya taifa pamoja na makumbusho nyengine nyingi duniani kote. Pia, tovuti ya eLucy ina kopi za picha za mifupa yote ya Dinknesh iliogunduliwa na unaweza kuilinganisha na mifupa ya vissukuku vingine vilivyogunduliwa. https://elucy.org/

 

Mantegaftot Sileshi, Yohannes Gebre Egziabher na Philipp Sandner wamechangia kuandika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.