Msukosuko wa Fedha katika spoti
21 Oktoba 2008Msukosuko wa fedha ulimwenguni, unazusha hofu kwamba athari zake zaweza pia kuenea katika nchi mbali mbali duniani.Na sio tu katika sekta ya uwekezaji,nafasi za kazi bali hata katika medani ya spoti au michezo.Na sio tu mchezo kama kabumbu ,bali pia kuanzia michezo ijayo ya olimpik 2012 mjini London, michezo ya Baseball na Basketball na golf nchini Marekani, hadi mbio za magari za Formula One barani Ulaya na nje yake.
Tuanze na Kabumbu au dimba:Matajiri tangu kutoka Marekani,Asia hata Urusi, wamekuwa wakinunua vilabu hasa vya Uingereza kama vile Manchester United na Chelsea.Kwa kuzuka msukosuko wa fedha hivi sasa, zile klabu za Ulaya ambazo hazikirimiwi na matajiri wakubwa ,zimeanza kukumbwa na baridi.Kwani, klabu hizo zimeanza kuathiriwa na kuporomoka kwa uchumi na zinaweza hata kudhurika zaidi kutokana na msukosuko uliozuka-alao katika kipindi kifupi kijacho.Hii ni kwa kuwa, wafadhili watapungua na mashabiki wanaonunua tiketi kwenda viwanjani pia watapungua .
David Triesman,rais wa Shirikisho la dimba la Uingereza (FA) amearifu kwamba mpira nchini Uingereza limekumbwa na deni la pauni bilioni 3 na kwamba haondoi uwezekano wa klabu mojawapo mashuhuri kuanguka.
Mkuu wa Premier League -Ligi ya Uingereza Richard Scudamore alisema mapema mwezi huu kwamba mfumo wa mchezo wa mpira unaweza kuendelezwa kama ulivyo licha ya msukosuko wa fedha uliozuka.
Shida zazoweza kuzuka kwa mfano kwa siku zijazo za klabu ya Manchester United iliofunga mkataba wa thamani ya pauni milioni 56.5 na kampuni la kimataifa la Marekani baada ya kampuni hilo kuokolewa kwa kiniinuamgongo cha serikali ya Marekani.
Klabu nyengine ya Premier League mbali na Manchester West ham United haijapata mfadhili wa jazi zake .Hii inafuatia kuanguka kwa kampuni la XL Leisure Group.Klabu iliopanda daraja ya kwanza ya West Bromwich Albion imeshindwa pia kumpata mfadhili mwengine wa kujaza pengo lililoachwa na kampuni la simu la Ujerumani Deutsche Tekom (T-Mobile).
Klabu ya Newcastle United ilikaribia kupoteza mkataba wake wa kutembeza katika jazi zake na Banki ya Nothern Rock ambayo ilibidi kuokolewa na serikali ya Uingereza .Lazio Roma ya Itali,ambayo ni klabu ya 6 kwa ukubwa humo nchini , hadi sasa haikupata mfadhili kwa jazi zake.
Lakini sio dimba tu linaloathirika na msukosuko wa fedha: Baseball,mchezo maarufu sana Marekani na hata Japan na Cuba, kuuzwa kwa timu ya Chicago Cubs kunaweza kukachelewa kutokana na msukosuko wa fedha isipokuwa mwenye kumiliki timu hiyo Tribune Co atakuwa tayari kuridhia bei ya chini zaidi kuuza Chicago Cubs.
Ama katika mchezo wa basketball-mpira wa kikapu -fedha pia zimeanza kupungua kwenye kikapu hicho.Ligi ya basketball nchini Marekani NBA imekumbwa pia na msukosuko huu wa fedha hadi kubidi kukata mashindano kadhaa yanayotangulia msimu mpya ambayo yalipangwa kuchezwa huku Ulaya mwaka huu.Hii ni kwa muujibu wa kamishna wa NBA David Stern alivyosema mapema mwezi huu.
NBA ikaamua mashindano 4 katika miji 4 ya ulaya kwa mwaka huu 2008 badala ya mashindano 7 katika miji 6 iliovyokuwa mwaka jana.Stern alitangaza kwamba NBA itwafukuza kazi watumishi wake 80 .
Mbio za magari za Formular-one chini ya paa la FIA lilipendekeza wiki iliopita kuchukuliwa hatua kali za kupunguza matumizi.Mabingwa wa zamani wa mbio hizi Williams ambao wamepatwa na hasara ya pauni milioni 21.4 mwaka jana na wanaodhaminiwa tangu na banki iliopewa kiinua-mgongo na serikali ya uingereza ya RBS na makampuni mali ya Banki ya Iceland ndio timu pekee ya mbio za magari isiofadhiliwa na mabilionea.Shirika la mbio za magari -FIA linahofia kwahivyo kuna hatari ya kweli hakutakua na wafadhili kwa baadhi ya magari.
Msukosuko huu wa fedha una faida zake upande mwengine:Jiji la London, mwenyeji wa michezo ijayo ya Olimpik ya majira ya kiangazi 2012 inayofuatia ile ya Beijing ya mwaka huu, litanufaika kutobid kutumia fedha nyingi sana kwa maandalio.Kuanguka kwa bei za majumba kutashawishi kutojengwa majumba mengi katika kijiji cha olimpik kwa kuhofia itakua vigumu baadae kuyauza.Idadi ya awali ya maskani 4,200 kwa imepunguzwa na kuwa 3000.
Msukosuko wa fedha utairuhusu serikali ya uingereza kuishawishi Halmashauri Kuu ya olimpik ulimwenguni kupunguza matumizi.