Msimu wa kushangaza na mabingwa wa kawai
29 Juni 2020Ligi hiyo imemaliza msimu wake katika viwanja vitupu na kuna matumaini madogo sana kwamba mashabiki wataruhusiwa viwanjani katika idadi kubwa mapema msimu ujao.
Afisa mkuu mtendaji wa kitengo cha DFL kinachosimamia ligi kuu Christian Seifert amesema ni wazi kwamba mwanzoni mwa msimu ujao mambo huenda yakawa vivi hivi akiongeza kuwa msimu huu wa joto utakuwa mgumu sana kwa vilabu vya Ulaya.
Mpango huo wa kanuni kali za usalama na usafi wa DFL na Shirikisho la Kandanda la Ujerumani – DFB umepata sifa kubwa ndani na nje ya Ujerumani, huku Bundesliga ikionekana kuwa kielelezo kwa ligi nyingine zilizorejeshwa baadaye.
Mbali na hayo, Bayern Munich waliendeleza udhibiti wao wa kandanda la Ujeurmani kwa kubeba taji lao la nane mfululizo. Msikilize nahodha Manuel Neuer akizungumza kuhusu kubeba ubingwa bila mashabiki "Hii ni hali mpya kabisa kwetu na hakuna anayetaka kupitia kitu kama hicho. lakini bila shaka bado tuna furaha kuwa tumekabidhiwa taji. Ulikuwa msimu mzuri kwetu. Tuna furaha kuwa sisi ni mabingwa wa Ujerumani kwa mara nyingine."
Borussia Moenchengladbach walijikatia tiketi ya nne ya kucheza Champions League na kuwapiku Bayer Leverkusen.
Kilichosisimua hata hivyo ni kivumbi cha kuepuka kushuka daraja, ambapo Werder Bremen walipata muujiza na kurefusha maisha yao ya miaka 39 katika Bundesliga kwa angalau siku nyingine 10.
Mabingwa hao mara nne wa Bundesliga waliwararua FC Cologne 6 – 1 Jumamosi na kutoka eneo la kushushwa daraja na kuwapiku Fortuna Duesseldorf ambao walifungwa 3 – 0 na Union Berlin na hivyo wakatumbukia katika ligi daraja la pili pamoja na Paderborn.
Kocha wa Bremen Florian Kohfeldt aliwaonea huruma Dusseldorf lakini pia akasema bado sio wakati wa kushangilia "Kwa wakati huu tunawaonea huruma Duesseldorf, ambao walicheza vizuri sana katika mzunguko wa pili, wakawa na mechi nyingi nzuri, kawaida walikuwa na mechia ambazo walipoteza pointi. Hata ingawa nina furaha, huruma yangu ni kwa wana Duesseldorf.
Bremen sasa watashuka dimbani dhidi ya Heidenheim mnamo Julai 2 na 6 katika mechi ya mchujo.
Heidenheim walimaliza katika nafasi ya tatu ya daraja la pili baada ya Mabingwa wa Ulaya na Ujerumani Hamburg SV kukosa nafasi nzuri ya kurejea katika daraja la kwanza kwa kubamizwa 5 – 1 na Sandhausen.
Hamburg walishuka ngazi miaka miwili iliyopita kwa mara ya kwanza katika historia ya Bundesliga.
Mabingwa ligi daraja la pili Arminia Bielefeld na VfB Stuttgart wamepandishwa daraja moja kwa moja.
Bayern Munich wanawinda mataji mawili kwa mara ya 13 katika msimu mmoja wakati watashuka dimbani na Bayer Leverkusen katika fainali ya Jumamosi ya Kombe la Shirikisho katika uwanja wa Olimpiki mjini Berlin. Ikumbukwe pia kuwa miamba hiyo ina fursa ya kubeba kombe la Champions League