1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msimamo wa mataifa ya Afrika kuhusu Zimbabwe wakosolewa

Abdulrahman, Mohamed21 Aprili 2008

Viongozi watakiwa kutokaa kimya.

https://p.dw.com/p/DldD
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe(Kulia) akiwa na mwenzake wa Afrika kusini Thabo Mbeki.Picha: AP

Licha ya shinikizo linaloongezeka kutoka baadhi ya mataifa makubwa ya magharibi kutaka umoja wa mataifa uingilie kati mgogoro kuhusu uchaguzi Zimbabwe, lakini uwezekano huo ni jambo linaloelekea kuwa mbali mno. Kwa hakika bado kuna viongozi wa mataifa jirani na Zimbabwe wenye kumlinda rais Robert Mugabe, akiwemo Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini.

Hali ya mvutano na tafauti ya misimamo juu ya nini kifanywe kuhusu Zimbabwe ilijitokeza wazi katika mkutano wa wiki iliopita kwenye umoja wa mataifa, kati ya umoja huo na wanachama wa umoja wa Afrika. Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini akipingana na wazo la Marekani na Uingereza kuushinikiza zaidi utawala wa Rais Mugabe na kuhusishwa kwa umoja wa mataifa katika mgogoro wa kisiasa nchini humo, alisema " suala hilo halina budi kuachiwa serikali ya Zimbabwe iamuwe yenyewe."

Huku dola hizo za magharibi zikiingiwa na wasi wasi kutokana na kucheleweshwa matokeo ya uchaguzi wa Machi 29 na serikali ya rais Mugabe inasema kuchelewa huko ni jambo la kawaida tu katika zoezi la uchaguzi. Tume ya uchaguzi ikasema haiwezi kutoa matangazo hadi kura zimehesabiwa upya katika majimbo 23 kama kilivyoomba chama tawala Zanu-PF-zoezi lililoanza Jumamosi iliopita. Itakumbukwa chama cha upinzani Movement for Democratic Change MDC kilishinda majimbo yote hayo na kikasema hatua hiyo ya tume ni mizengwe kutaka kubadili matokeo.

Rais wa Afrika kusini Thabo Mbeki alipewa jukumu la kuzipatanisha ZANu-PF na MDC baada ya mgogoro wa kisiasa kuzuka katika uchaguzi wa rais 2000, lakini sasa upinzani unasema amepoteza uaminifu kwa sababu ya matamshi yake kuhusu kucheleweshwa matokeo katika uchaguzi wa hivi karibuni. Mbeki alisema haoni kama kuna mgogoro Zimbabwe.

Mbeki na Mugabe ni marafiki wa chanda na pete tangu enzi za vita vaya ukombozi-pale Afrika kusini ilipokua chini ya utawala wa kibaguzi wa wazungu wachache na Zimbabwe ilipokua ikitawaliwa na walowezi wakiongozwa na Ian Smith na kujulikana wakati huo kama Rhodesia.

Kiongozi wa MDC Morgan Tsvangirai ambaye anaishi kwa wakati huu uhamishoni nchini Botswana kwa kile kinachotajwa sababu za usalama, anadai chama chake kimeshinda sio tu viti vya bunge bali kata urais anaipinga hoja ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi wa rais akisema ushindi wake umevuka kidogo asili mia 50 inayohitajika. Mugabe anamshtumu Tsvangirai akisema ni kibaraka wa nchi kubwa za magharibi-Marekani na Uingereza ambazo pamoja na umoja wa ulaya zimesisitiza matokeo hapana budi yatangazwe haraka.

Mataifa ya kiafrika yamekaa kimya, licha ya umoja wa Afrika kutoa taarifa mapema juma hili kutaka matokeo yatangazwe haraka. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice amesema ni wakati sasa kwa Afrika kuwa na msimamo ulio wazi. Hata katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan ametoa taarifa ya kusikitishwa na msimamo wa mataifa ya kiafrika akisema " Wakati shinikizo la kimataifa likizidi, waafrika wanafanya nini, wako wapi viongozi na nchi jirani."

Wadadisi wanasema hatua ya upande mmoja ya umoja wa mataifa pekee kuhusu Zimbabwe haiwezi kuzaa matunda bila ya uungaji mkono na mshikamano wa nchi za kiafrika na hasa zilizo jirani na Zimbabwe. Kushindwa kuafikiana katika kikao cha umoja wa mataifa na umoja wa Afrika kunadhihirisha ugumu wa mafanikio hayo.

Tatizo jengine ni misimamo ya Urusi na China, wanachama wa baraza la usalama. Kinyume na Marekani na Uingereza, Urusi na China zilijizuwia kutoa taarifa yoyote juu ya Zimbabwe, huku maafisa wa kibalozi wakisema jumuiya za kimkoa kama umoja wa Afrika zinaonyesha utayarifu wa kuitatua mizozo ya bara hilo.