"Msiba mkubwa kwa sera za ulinzi wa hali ya hewa"
17 Desemba 2007Wahariri hawaridhiki juu ya masharti yaliyokubaliwa ambayo, kwa maoni yao, si makali vya kutosha. Kwanza ni yaliyoandikwa na “Berliner Zeitung”:
“Tukiangalia uzito wa matatizo wa hali ya hewa, utatuzi uliyokubaliwa huko Bali hautoshi. Maafikiano hayaweki masharti ya kulazimisha kwa nchi za kiviwanda kupunguza utoaji wa gesi chafu wala hayasemi nani achangie kwa kiasi gani katika utunzaji wa hali ya hewa.”
Moja kwa moja tuendelee na gazeti la “Tageszeitung la mjini Berlin” ambalo limetoa hukumu kali juu ya wajumbe wa mkutano huo:
“Mkutano wa Bali ni msiba mkubwa kwa sera za ulinzi wa hali ya hewa duniani. Katika hotuba zao, mawaziri na viongozi wa ujumbe wote walisisitiza vile uchunguzi wa wanasayansi kuhusu hali ya hewa unavyotia hofu na kwamba ni muhimu sana hatua zichukuliwe. Baadaye lakini katika mazungumzo walikataa hata herufi moja kwenye hati ilibadilishwe. Picha inayopatikana basi ni kwamba kwa kweli, hali ya hewa haipewi kipaumbele.”
Mhariri wa “Frankfurter Rundschau” katika uchambuzi wake anakumbusha kuhusu kuhusishwa kwa nchi zinazoendelea. Ameandika:
“Tukio muhimu zaidi la mkutano wa Bali ni kuzingatiwa kwa nchi zinazoendelea na nchi zinazobadilika kuwa nchi za kiviwanda kama China na India, hata ikiwa maneno yaliyotumika hayana uzito sana. Hadi sasa kuhusishwa kwao hakukufikiriwa, lakini bila wao haitawezekana kupunguza utoaji wa gesi ya Carbondioxide. Tulio nao sasa ni mfumo wa mpango wa kugharamia hatua za utunzaji wa hali ya hewa, teknolojia za kisasa na utunzaji wa misitu. Kazi sasa ni kujaza mfumo huo. Haya tayari ni mafanikio. Na yule ambaye alifuatia dakika za mwisho za mkutano wa Bali ambapo karibu mkutano ufeli, atakiri kuwa kweli ni mafanikio.”
Ni gazeti la “Frankfurter Rundschau”. Mhariri wa “Neue Osnabrücker Zeitung” naye anatathmini hivi mkutano huu juu ya hali ya hewa:
“Mazungumzo ya Bali yameonyesha wazi vile tofauti kati ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea ni kubwa – licha ya msaada na ushirikiano ulioahidiwa. Anayetaka kuziba pengo hili anapaswa kutafuta njia mpya bila ya kufikiria biashara tu. Wakaazi wa nchi za kiviwanda walizoea ustawi wao wa kuweza kununua kila kitu. Ikiwa lakini ununuzi wa bidhaa utakuwa kipimo cha maendeleo katika nchi zinazoendelea, sayari yetu basi hatimaye kweli itaharibika.”
Na hatimaye kwa ufupi tu ni gazeti la “Südwest Presse” kuhusu msimamo wa Marekani:
“Rais George Bush anapenda kujifanya kama mpiganaji aliye peke yake. Hajawahi kutengwa kama kwenye mkutano huo wa Bali. Na ingawa ni yeye aliyekubali mwisho, lakini amelaumu makubaliano hayo kwa kutokuwa mazito. Hivyo basi amepoteza kabisa imani kama kiongozi wa nchi yake.”