1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Ugaidi

Mshukiwa wa shambulizi la Sinagogi Marekani ahukumiwa kifo

3 Agosti 2023

Dereva mmoja wa lori Mmarekani amehukumiwa kifo kwa kuwauwa waumini 11 wa Kiyahudi miaka mitano iliyopita katika shambulizi baya zaidi la chuki dhidi ya Wayahudi nchini Marekani

https://p.dw.com/p/4Uiic
USA Robert Bowers zum Tode verurteilt
Picha: AFP

Dereva mmoja wa lori Mmarekani amehukumiwa kifo kwa kuwauwa waumini 11 wa Kiyahudi miaka mitano iliyopita katika shambulizi baya zaidi la chuki dhidi ya Wayahudi kuwahi kufanywa katika historia ya Marekani.

Baraza la wazee wa mahakama lenye wanachama 12 lilikubaliana kwa kauli moja kwamba Robert Bowers anapaswa kunyongwa kwa kuwauwa watu hao mnamo Oktoba 27, 2018 kwa kuwafyatulia risasi mjini Pittsburgh.

Soma pia: Afisa wa polisi awaua watu wanne katika sinagogi, Tunisia

Mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 50 alipatikana na hatia mwezi Juni ya mashtaka yote 63 yaliyowasilishwa dhidi yake, ikiwemo uhalifu wa chuki uliosababisha mauaji na jaribio la mauaji.

Wizara ya Sheria ya Rais Joe Biden hata hivyo imeweka zuio la adhabu ya kunyongwa, kumaanisha kuwa haijulikani kama hukumu hiyo itawahi kutekelezwa dhidi ya Bowers au la.

Bowers aliwafuatilia wahanga hao katika sinagogi, na kuwapiga risasi mara nyingi huku akipiga kelele na kusema "Wayahudi wote lazima wafe!"