Mshukiwa wa mauaji ya Shinzo Abe apandishwa mahakamani
13 Januari 2023Waendesha mashitaka nchini Japan wamemshitaki rasmi mshukiwa katika mauaji ya waziri mkuu wa zamani, Shinzo Abe. Tetsuya Yamagami amefunguliwa mashitaka ya mauaji na sasa kesi yake itaanza rasmi mahakamani. Yamagami pia ameshitakiwa kwa kuvunja sheria ya udhibiti wa bunduki, kwa mujibu wa mahakama ya wilaya ya Nara. Mmoja wa mawakili wake, Masaaki Furukawa, amesema Yamagami atalazimika kuwajibikia madhara ya vitendo vyake na kuwa mawakili wake wa utetezi watafanya kila wawezalo kupunguza adhabu atakayohukumiwa.
Mshukiwa huyo alikamatwa mara tu baada ya kudaiwa kumpiga risasi Abe kwa bastola ya kujitengenezea mwenyewe wakati kiongozi huyo wa zamani alipokuwa anatoa hotuba ya kampeni mwezi Julai nje ya kituo cha treni mjini Nara, magharibi mwa Japan. Yamagami aliwaambia polisi alimuuwa Abe kwa kuwa alikuwa na mahusiano na kundi la kidini alilolichukia.