1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshukiwa wa mauaji Afghanistan 'alichanganyikiwa' kurejeshwa vitani

16 Machi 2012

Mwanajeshi wa Marekani anayetuhumiwa kwa kuwauwa raia 16 Kusini mwa Afghanistan alifadhaishwa kuhusu kulepelekwa vitani kwa mara ya nne bila ya yeye kutarajia, lakini familia yake ilishtushwa na mauaji hayo.

https://p.dw.com/p/14LTl
Afghanistan NATO ISAF Helikopter Absturz

Wakili wa mshukiwa huyo John Henry Browne ameliambia shirika la habari la AP kuwa mteja wake alikuwa amehakikishiwa kuwa hangepelekwa tena katika eneo la mapigano.

Browne amesema mwanajeshi huyo pamoja na familia yake walikuwa wameambiwa kuwa safari zake za Mashariki ya Kati zilikuwa zimekwisha. Mwanajeshi huyo mwenye umri wa miaka 38 alikuwa tayari amejeruhiwa mara mbili katika safari zake tatu alizokuwa nchini Iraq.

Vizingiti kwa Marekani

Wakati huo huo Kampeni ya Marekani nchini Afghanistan imepata pigo mara mbili. Kwanza kundi la Taliban limesitisha mazungumzo kati yao na Marekani, na pili, Rais Hamid Karzai amesema Jumuiya ya NATO inafaa kuondoka maeneo ya vijijini na kuharakisha shughuli ya kuyakabidhi majeshi ya Afghanistan majukumu ya kiusalama katika nchi nzima.

Marekani imesema itaendelea kuunga mkono juhudi za amani
Marekani imesema itaendelea kuunga mkono juhudi za amaniPicha: Reuters

Hatua hizo ni vizingiti katika mkakati wa Marekani wa kumaliza vita vya miaka kumi nchini humo katika wakati ambapo uungaji mkono wa mzozo huo unapungua. Sehemu ya mpango wa Marekani kuondoka ni kuyakabidhi mamlaka vikosi vya Afghanistan japo kwa hatua. Mpango mwingine ni kuwashirikisha Wataliban katika mazungumzo ya kisiasa na serikali ya Afghanistan, ijapokuwa haijabainika ikiwa kumekuwa na mafanikio yoyote tangu mwezi Januari.

Karzai akariri mwito wake

Karzai alisema anataka wanajeshi wa Afghanistan wachukue usukani wa nchi nzima ifikapo mwaka 2013, katika kile kilichoonekana kuwa ni hatua ya kishinikiza Marekani kuondoka nchini humo mapema na ilivyopangwa.

Taarifa kutoka ofisi ya Karzai ilisema kuwa wakati wa mkutano wake na Waziri wa Ulinzi wa Marekani aliyezuru nchini humo Leon Panetta, rais huyo alisema vikosi vya usalama vya Afghanistan vina uwezo wa kutoa ulinzi katika vijiji nchini humo. Karzai aliyasema hayo wakati wabunge wa Afghanistan wakionyesha hasira yao baada ya mwanajeshi wa Marekani anayedaiwa kuwauwa raia 16, kuhamishiwa Kuwait. Walitaka mshukiwa huyo ashitakiwe nchini humo.

Jana Alhamisi mwanajeshi mmoja wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO aliuwawa katika shambulio la bomu la kutegwa kando ya barabara Mashariki mwa Afghanistan. Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu uraia wa mwathiriwa huyo.

Kuhamishwa mshukiwa wa mauaji kumeibua hasira Afghanistan
Kuhamishwa mshukiwa wa mauaji kumeibua hasira AfghanistanPicha: dapd

Taliban wasitisha mazungumzo na Marekani

Licha ya taarifa ya Taliban kuwa imesitisha mazungumzo na Marekani, msemaji wa Ikulu ya Rais Jay Carney alisema Marekani itaendelea kuunga mkono mpango wa upatanishi unaoongozwa na Afghanistan. Taarifa ya msemaji wa Taliban Zabiullah Mujahid iliishutumu Marekani kwa kushindwa kutimiza ahadi zake, kutoa masharti mapya, na kutoa madai ya uwongo kuwa kundi hilo la wanamgambo linafanya mazungumzo sambamba na washirika wengine.

Mujahidi amesema kundi hilo hivyo basi limesitisha mazungumzo hayo yanayoandaliwa Qatar hadi pale Marekani itakapofafanua msimamo wao kuhusu masuala hayo na kutimiza ahadi zao.

Mwandishi: Bruce Amani/AP

Mhariri:Josephat Charo