Mshukiwa wa kashfa ya rushwa ndani ya EU kutoboa siri zote
18 Januari 2023Mtu anayechukuliwa kama kinara wa kundi linalotuhumiwa kupokea rushwa kutoka Moroko na Qatar ili kushawishi sera za Umoja wa Ulaya kuelekea nchi hizo, ameahidi kutoboa siri zote ili apewe adhabu ndogo.
Mtu huyo, Pier Antonio Panzeri mwezi uliopita alishitakiwa kwa makosa ya rushwa, utakatishaji wa fedha na kuwa mwanachama wa kundi la kihalifu, na mawakili wake wamesaini nyaraka ambamo anakiri makosa hayo na kuyajutia.
Katika nyaraka hizo Panzeri anakubali kuwaambia waendeshamashtaka namna mpango wao ulivyoendeshwa, namna fedha zilivyotolewa na nchi husika, na majina ya wote walionufaika katika kashfa hiyo ya ubadhirifu.
Kulingana na waranti wa kumkamata uliotolewa na Ubelgiji, Panzeri anashukiwa kuwarubuni wajumbe wa Bunge la Ulaya kwa fedha ili waingilie kisiasa katika masuala yanayohusu Qatar na Moroko. Nchi hizo mbili zimejitenga mbali na madai hayo.